Mgombea Ubunge wa Jimbo la
Bukombe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Doto Mashaka Biteko amesema
CCM imepanga kuongeza kasi ya maendeleo katika Kata ya Namonge kwa kusogesa
karibu huduma za jamii.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba
18, 2025 wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Namonge wilayani Bukombe
mkoani Geita ikiwa ni sehemu Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“ Hapa tuna vitongoji sita kati
yake vitatu havina umeme, mkituchagua tutakamilisha umeme katika vitongoji
vyote, tunataka kila nyumba iwe na umeme, amesema Dkt. Biteko
Akizungumzia huduma za afya
amesema “ Nataka nimwambie Mtendaji wa Kata hii hatutaki vikao vya muda mrefu
wananchi hawa wanahitaji huduma, nimenunua vifaa kwa ajili ya zahanati
ningependa kuona imekamikika na inatoa huduma kwa wananchi ili wasitembee
kilomita 12 kufuata huduma.”
Aidha, amesema Kata hiyo imepiga
hatua kimaendeleo ambapo awali kulikuwa na shule saba za msingi na sasa zipo
14, kuna shule mbili za sekondari kutoka moja pamoja na kituo kikubwa cha afya
ambacho upasuaji tayari umeanza kufanyika.
Dkt. Biteko ametaja mipango ya
CCM kwa miaka mitano ijayo katika Kata hiyo kuwa ni kujenga shule katika maeneo
yasiyo na huduma hiyo pamoja na kuongeza ujenzi wa zahanati Mji mwema na Bugega
sambamba na kukamilisha zahanati ya Ilyamchele.
Ameendelea kusema kuwa maendeleo
ya Namonge yametokana na upendo wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa
akitoa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo hivyo amewahimiza wananchi hao
kujitokeza kwa wingi na kumpigia kura ili aweze kuendeleza jitihada za
maendeleo katika Kata yao.
Naye, Mgombea wa Udiwani Kata ya
Namonge, Mlalu Bundala amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi
wa Dkt. Samia na Biteko wamesaidia kujenga daraja, Shule ya Msingi Ilyamchele,
Shule ya Sekondari Said Mkumba pamoja na kujenga barabara ya Ilyamchele hadi
Nyamagana.
Amesema kuwa mafanikio hayo
yametokana na jitihada zao za kuwaletea maendeleo wananchi wa Namonge na hivyo
Oktoba 29 mwaka huu wajitokeze kwa wingi na
kuwapigia kura wagombea wa CCM.
Katika hatua nyingine,
akizungumza na wananchi wakati akiendelea na kampeni katika Kata ya Bulega,
Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali inatekeleleza miradi ya maendeleo ikiwemo
mradi wa maji, wamechimba visima vitano, kujenga zahanati pamoja na
kupeleka umeme katika vijiji vyote.
Aidha, amesema wanahitaji
kuongeza nguzo za umeme na kuwa wakichaguliwa
Oktoba 29 watafanya hivyo ikiwa ni pamoja na kuendeleza programu ya
kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia wkatika Wilaya ya Bukombe.
“ Ni lazima tuongeze shule hapa
ya kidato cha tano na sita ili watoto wanaotoka maeneo mengine pia wapate fursa
ya kusoma hapa,” amesoma Dkt. Biteko.
Amesisitiza kuwa endapo
wakichaguliwa tena watahakikisha wanajenga soko, barabara pamoja na kukarabati
shule chakavu.
“ Dkt. Samia ametoa fedha ya
kujenga barabara ya lami kutoka Ushirombo kwenda Katoro hadi Geita, nataka
nimuombe tena fedha kwa ajili ya kujenga shule ya kidato cha tano na sita sasa
ili kazi hii ifanyike nawaomba msiniangushe, Oktoba 29 mkampigie kura Dkt.
Samia ,” amesema Dkt. Biteko
Kwa upande wake, Diwani wa Kata
ya Bulega, Erick Kagoma amesema kuwa kwa miaka 10 Kata hiyo imepiga hatua ya
maendeleo kwa kutekeleza ilani ya CCM.
Ambapo wamejenga shule za msingi
mpya tatu, wameongeza umeme kutoka vitongoji viwili hadi nane pamoja na
kuboresha barabara kadhaa katika Kata hiyo.
“ Sasa tumekuja kwenu kuomba
ridhaa ili mimi, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Biteko tuweze kutekeleza ilani
ya CCM kwa kujenga shule, hospitali, kuweka umeme hivyo naomba mtuchagu,”
amesema Kagoma.
0 Maoni