Dkt. Abbasi aitaka Menejimenti Ngorongoro kusimamia uwajibikaji

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, ameitaka Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kuendelea kusimamia uwajibikaji miongoni mwa watumishi wake kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni, ili kuhakikisha malengo ya Serikali katika sekta ya uhifadhi na utalii yanafikiwa.

Dkt. Abbasi alitoa wito huo Septemba 18, 2025, alipotembelea makao makuu ya Mamlaka hiyo mkoani Arusha katika ziara ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo Makumbusho ya Jiolojia na ujenzi wa jengo jipya la ofisi za Makao Makuu ya Ngorongoro.

Akizungumza katika kikao na menejimenti ya Mamlaka hiyo, Dkt. Abbasi alisisitiza kuwa kila mtumishi wa umma anapaswa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na weledi kwa lengo la kuleta tija kwa taifa.

“Simamieni watumishi walio chini yenu katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi,” alisema Dkt. Abbasi.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii katika Mamlaka hiyo, Joas Makwati, alisema kuwa Mamlaka imejipanga kuboresha huduma mbalimbali kwa lengo la kukuza uhifadhi wa maliasili, kuimarisha sekta ya utalii pamoja na kuongeza mchango katika maendeleo ya wananchi wanaoishi katika maeneo jirani na hifadhi.




Chapisha Maoni

0 Maoni