Kamishna wa Uhifadhi Shirika la
Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA Musa Nassoro Kuji, amewataka Watumishi
wa Kampuni Tanzu ya TANAPA (TANAPA Investment Ltd - TIL) kuongeza ubunifu na
kuchapa kazi kwa ufanisi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia
katika utoaji wa huduma za ukandarasi ndani na nje ya Shirika.
Kamishna Kuji ameyasema hayo jana
Septemba 18, 2025 katika kikao chake na watumishi wa kampuni hiyo tanzu ya
TANAPA.
TIL ni Kampuni tanzu ya TANAPA
iliyoanzishwa mnamo mwaka 2019 na lengo likiwa ni kutoa msukumo katika
utekelezaji wa miradi ya Shirika pamoja na kuwa Kitega Uchumi cha Shirika
katika kutekeleza miradi ya nje ya Shirika.
Kamishna Kuji ametumia fursa hiyo
kuipongeza kampuni hiyo kwa kazi ambazo imeshazifanya ikiwemo ukarabati wa
barabara ya Hifadhi ya Taifa Arusha, ukarabati wa kiwango cha changarawe wa
baadhi ya barabara za Jijini Arusha, ukarabati wa kipande cha barabara ya
Hifadhi ya Taifa Serengeti na kazi nyingine ambazo zimetekelezwa kwa ufanisi.
“Pokeeni pongezi kutoka kwa Bodi
ya Wadhamini ya Shirika na Bodi imenituma niwaeleze kuwa inayo matarajio makubwa
sana kwenu na hivyo msiwaangushe. Endeleeni kufanya kazi kwa weledi, bidii,
nidhamu, kujituma, ushirikiano, upendo na mshikamano ili muweze kutimiza
malengo ya kuanzishwa kwa TIL” alisema Kamishna Kuji.
Naye, Mtendaji Mkuu wa TIL,
Mhandisi Dkt.Richard Matolo alitoa pongezi zake kwa Kamishna Kuji kwa kutenga
muda wake na kuja kuzungumza na watumishi wa kampuni hiyo na kuahidi kuchapa
kazi kwa ari na kasi zaidi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na bodi ya
wadhamini kupitia kampuni hiyo.
Kampuni Tanzu ya TANAPA ni nyenzo
muhimu katika kuhakikisha kuwa miundombinu ya uhifadhi na utalii pamoja na ya
kiutawala zilizopo ndani ya Hifadhi za Taifa Tanzania inakuwa katika hali
nzuri wakati wote.
Na. Edmund Salaho - Arusha
0 Maoni