Rais wa
zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela
baada ya kupatikana na hatia ya kula njama ya uhalifu katika kesi inayohusiana
na kupokea fedha haramu mamilioni ya euro kutoka kwa aliyekuwa kiongozi wa
Libya, hayati Kanali Muammar Gaddafi.
Uamuzi
huo umetolewa Alhamisi na Mahakama ya Jinai ya Paris, ambayo hata hivyo
ilimuondolea mashtaka mengine ya rushwa ya kupokea na ufadhili haramu wa
kampeni za kisiasa.
Kwa
mujibu wa hukumu hiyo, Sarkozy atalazimika kuanza kutumikia kifungo hicho mara
moja, hata kama atakata rufaa, jambo ambalo tayari ametangaza kuwa atalifanya.
Akizungumza
nje ya mahakama baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Sarkozy mwenye umri wa miaka
70, alisema uamuzi huo ni “muhimu mno kwa utawala wa sheria”, na kusisitiza
kuwa kesi hiyo ina nia ya kisiasa dhidi yake.
Sarkozy
alihudumu kama Rais wa Ufaransa kati ya mwaka 2007 na 2012. Anadaiwa kupokea
fedha haramu kutoka kwa Gaddafi kwa ajili ya kufadhili kampeni yake ya uchaguzi
mwaka 2007.
Upande wa
mashtaka ulidai kuwa Sarkozy aliahidi kumsaidia Gaddafi kusafisha taswira yake kuwa
mtu asiyehitajika katika mataifa ya Magharibi, kama sharti la kupokea msaada
huo wa kifedha.
Hukumu
hiyo imekuwa pigo kubwa kwa rais huyo wa zamani, ambaye kwa miaka kadhaa
amekuwa akikabiliwa na tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa sheria wakati wa
uongozi wake.
0 Maoni