NCAA yahamasisha utalii wa kupanda milima kupitia Mlima Lomalasin

 

Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya utalii, imeadhimisha Siku ya Utalii Duniani kwa kuhamasisha utalii wa kupanda milima kupitia Mlima Lomalasin, uliopo ndani ya eneo la hifadhi hiyo maarufu duniani.

Maadhimisho hayo yaliyofanyika jana Septemba 27, 2025, yamelenga kutangaza vivutio vya utalii wa asili vinavyopatikana ndani ya Ngorongoro, huku Mlima Lomalasin ukielezwa kuwa moja ya vivutio vinavyoibukia kwa kasi katika eneo hilo.

Mlima huo unaotajwa kuwa wa tatu kwa urefu nchini Tanzania, una urefu wa mita 3,682 kutoka usawa wa bahari na umekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wanaopenda utalii wa milima kutokana na mandhari yake ya kuvutia na mazingira asilia yaliyohifadhiwa vyema.

Akizungumza wakati wa shughuli ya kupanda mlima huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Huduma za Utalii na Masoko NCAA, Mariam Kobelo, alisema maadhimisho ya mwaka huu yamelenga kuhamasisha utalii wa ndani kupitia mazao mbadala ya utalii.

"Leo tunapoadhimisha Siku ya Utalii Duniani, tunatumia fursa hii kutangaza Mlima Lomalasin na kuhamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki katika utalii wa kupanda milima. Huu ni mlima wa kipekee unaotoa fursa ya kuona mandhari nzuri ya asili, sambamba na kuutangaza utalii wa kiikolojia," alisema Kobelo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Land Africa Safaris, Bw. Timothy Mdinka, alisema Mlima Lomalasin una upekee wa kipekee kijiografia na kwamba umeendelea kuwavutia wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.

"Mlima huu upo katika eneo la kipekee kijiolojia linalounganisha vivutio vingine muhimu kama Kreta ya Empakai, Kreta ya Olmoti, Mlima Losirwa, Oldoinyo Lengai na eneo la kihistoria la Engaruka. Hii inaufanya kuwa kivutio cha kipekee kwa watalii wa ndani na wa kimataifa," alisema Mdinka.

Siku ya Utalii Duniani huadhimishwa kila mwaka Septemba 27 kwa lengo la kuhamasisha maendeleo ya utalii endelevu na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Utalii na Mageuzi Endelevu."

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wadau mbalimbali wa utalii wakiwemo wawakilishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, kampuni za utalii ikiwemo Land Africa Safaris, Asante Tours, Crater Lodge, Azam TV, Nols & Beyond pamoja na wakazi wa Kijiji cha Bulati ambacho kimebarikiwa kuwa mwenyeji wa Mlima Lomalasin.




Chapisha Maoni

0 Maoni