Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Agosti 11, 2025 amemwakilisha Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya Spika mstaafu wa Bunge la
Tanzania, Job Yustino Ndugai, yaliyofanyika shambani kwake, kijiji cha
Msunjulile, wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Akizungumza katika ibada ya mazishi, Waziri Mkuu amewataka Watanzania
kuenzi mema yote yaliyofanywa na Hayati Ndugai enzi za uhai wake, akisema
mchango wake katika uongozi wa Bunge na Taifa kwa ujumla utabaki kuwa
kumbukumbu muhimu kwa vizazi vijavyo.
Amesema kuwa akiwa mwakilishi wa wananchi wa Kongwa, Hayati Ndugai ametoa
mchango mkubwa katika kipindi cha miaka 20 ya utumishi wake, na kwamba wote ni
mashuhuda wa maendeleo makubwa yaliyopatikana katika sekta mbalimbali za
maendeleo pamoja na huduma za kijamii. “Serikali itaendelea kumuenzi kwa yale
yote aliyoyafanya kwa wanaKongwa.”
Aidha, Waziri Mkuu ameeleza kuwa hayati Ndugai alikuwa mlinzi wa taratibu
za Bunge na mshirika wa karibu katika kuimarisha ushirikiano kati ya Bunge na
Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa, akisisitiza mawasiliano ya uwazi,
mshikamano na mwelekeo wa pamoja wa utekelezaji wa ajenda za kitaifa.
Vilevile, Mheshimiwa Majaliwa amemtaja Hayati Ndugai kama kiongozi mwenye
weledi, uadilifu, unyenyekevu, na mchapakazi ambaye alibeba heshima ya mkoa wa
Dodoma na jimbo la Kongwa kupitia uongozi na siasa za uwajibikaji.
Pia, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itasimamia utekelezaji wa maagizo
yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ya kukamilishwa kwa masuala yote
yaliyoanzishwa na Hayati Ndugai, pamoja na kuendeleza makumbusho ya Kongwa
ikiwa ni kielelezo cha kupigania uhuru kwa nchi za kusini mwa afrika.
“Tutasimamia agizo hili kwa ukamilifu.”
Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto
Biteko, ametoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa Kongwa na
Watanzania wote kwa ujumla kutokana na
msiba wa hayati Ndugai.
Naye, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa wanaamini katika
kumuenzi hayati Ndugai na watamkumbuka daima kwa kuendeleza misingi pamoja na
mambo mema yote aliyoyatenda wakati wa uhai wake.
Mazishi ya Hayati Ndugai yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo
Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi Zena Saidi,
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongela, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda,
viongozi wengine kitaifa, ndugu, jamaa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali.
Hayati Job Ndugai alifariki Agosti 06, 2025 jijini Dodoma kwa Shinikizo
la damu lililoshuka sana.
0 Maoni