Waziri wa Maliasili na
Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) ametoa wito kwa watanzania wa kada
mbalimbali kutembelea maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa viwanja vya
nzuguni Jijini Dodoma pamoja na maeneo mengine nchini ili waweze kupata elimu
ya vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo mbalimbali yaliyohifadhiwa.
Waziri Chana ametoa
maelezo hayo akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea banda la Wizara
ya Maliasili na Utalii katika maonesho ya wakulima nanenane yanayofanyika
kitaifa viwanja vya Nzughuni Dodoma ambapo wizara ya Maliasili na Utalii na
taasisi zake inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutangaza vivutio vya
utalii, kutoa elimu ya shughuli za uhifadhi, fursa za uwekezaji na maendeleo ya
jamii.
“Natoa wito kwa
watanzania kutembelea maonesho ya nanenane katika kanda zote yanapofanyika ili
wapate elimu ya vivutio vya utalii tulivyonavyo, fursa za uwekezaji, elimu ya
uhifadhi, na ufugaji nyuki. Wizara inaendelea kuongeza mazao mbalimbali ya
utalii ikiwemo utalii wa vyakula na utalii wa kilimo kwa kuwa maonesho haya
yamefunganisha sekta mbalimbali ili tuendelee kutangaza nchi yetu na kupata
maendeleo kwa pamoja,” aliongeza Balozi Chana.
Mamlaka ya Hifadhi ya
eneo la Ngorongoro (NCAA) inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutangaza vivutio
vya utalii kama vile Kreta za Ngorongoro, empakai, Olmoti, mlima Lolmalasin
ambao ni wa tatu kwa urefu Tanzania, maporomoko ya maji endoro sambamba na
mapango ya Tembo.
Vivutio vingine
vinavyotangazwa katika maonesho hayo ni pamoja na Utalii wa malikale kama Makumbusho ya Olduvai, Nyayo za
Laetoli, mchanga unaohama, utalii wa anga katika Kimondo cha Mbozi na Mapango
ya Amboni Tanga yenye historia mbalimbali ikiwemo harakati za kudai uhuru wa
Tanzania bara urithi na utamaduni wa makabila na watu wa Tanga.
Wageni wanatakaotembelea
banda la Wizara ya Maliasili na Utalii pia watapata fursa ya kushuhudia
mubashara vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro kupitia "TV Screen"
kubwa iliyofungwa kwenye banda hilo.
Kauli mbiu ya maonesho ya
nanenane kwa mwaka 2025 ni “Chagua viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya
kilimo, mifugo na Uvuvi”.
0 Maoni