WAKALA ya Barabara za
Vijijini na Mjini (TARURA) umesema kuwa tangu kuanzishwa kwake, wamefanikiwa
kujenga jumla ya madaraja 439 ya mawe yenye thamani ya bilioni 15, hatua ambayo
imewezesha kuokoa kiasi kikubwa cha fedha.
Hayo yamebainishwa leo
jijini Dodoma na Mhandisi Mshauri wa TARURA, Mhandisi Pharles Ngeleja, wakati
akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea
mkoani hapa.
Akizungumza kuhusu
mafanikio hayo, Mhandisi Ngeleja ameleza kuwa, ujenzi wa madaraja ya mawe
unatoa nafuu kubwa ya gharama, na unazingatia mabadiliko ya hali ya hewa ambayo
huathiri miundombinu mingine.
"TARURA tumeona
umuhimu wa kutumia teknolojia ya madaraja ya mawe, ambayo ni nafuu na inaendana
na mazingira ya vijijini. Kwa madaraja haya 439, tumetumia bilioni 15. Ikiwa
tungetumia njia ya ujenzi wa madaraja ya zege, tungeweza kutumia zaidi ya bilioni
90. Hivyo, ujenzi wa madaraja ya mawe umewezesha kuokoa kiasi kikubwa cha fedha
za serikali," amesema Mhandisi Ngeleja.
Aidha, Mhandisi
Ngeleja amezungumzia umuhimu wa miundombinu ya barabara katika kusaidia
maendeleo ya kilimo akisisitiza kwamba, kupitia ujenzi wa miundombinu bora,
wakulima wanaweza kufikia masoko kwa urahisi, jambo ambalo linachangia katika
kuongeza kipato na kuboresha uchumi wa maeneo ya vijijini.
"Kama mnavyojua,
TARURA ndiyo mshipa wa damu wa wakulima. TARURA inawawezesha wakulima kufika
kwenye masoko kwa urahisi. Hata kama mkulima alime kwa kiasi kikubwa, kama hana
barabara, hawezi kufikia malengo yake. Hivyo, miundombinu bora ya barabara ni
muhimu katika kuleta maendeleo ya kilimo na kuongeza uzalishaji,"
ameongeza.
Katika maonesho ya
Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, TARURA imekuwa mstari wa mbele katika
kutoa elimu na kuonyesha mafanikio yake katika kuboresha miundombinu ya
barabara na madaraja, jambo ambalo linasaidia kuboresha maisha ya wananchi na
kuongeza fursa za maendeleo katika maeneo ya vijijini.
0 Maoni