WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa ametoa wito kwa Wakuu wa Taasisi za Kupambana na Rushwa wa Jumuiya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika
(SADC) kuendelea kusimamia kikamilifu na kwa ufanisi utekelezaji wa Itifaki ya
Jumuiya hiyo dhidi ya Rushwa ili kujenga ukanda usio na Rushwa.
Amesema kuwa Itifaki ya
SADC Dhidi ya Rushwa bado ni nyenzo muhimu katika kufanikisha utawala bora,
amani na muungano endelevu wa kikanda hivyo viongozi hao wanapaswa kuhakikisha
kuwa juhudi za kupambana na rushwa zinaendelezwa.
Ametoa wito huo leo
(Agosti 04, 2025) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwenye Ufunguzi wa Maadhimisho ya miaka 20 ya Utekelezaji wa Itifaki ya Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika Dhidi ya Rushwa, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa
Mikutano wa Hoteli ya Gran Melia, jijini Arusha.
“Lazima tukiri kwamba
rushwa ni tishio kwa usalama. Inachochea uhalifu uliopangwa, usafirishaji
haramu wa binadamu, ugaidi, na kudhoofika kwa utawala wa sheria.”
Aidha, Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa katika kipindi cha hivi karibuni, nchi Wanachama wa SADC
ikiwemo Tanzania zimeendelea kuimarisha sheria za mapambano dhidi ya rushwa,
kuziwezesha Taasisi zinazosimamia udhibiti na mapambano dhidi ya rushwa pamoja
na kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari za rushwa kwa ustawi wa Taifa.
“Hata ushirikiano wa
kikanda katika mapambano dhidi ya rushwa umeimarika kwa kubadilishana taarifa,
mashirikiano katika masuala ya sheria pamoja na uchunguzi wa pamoja katika
kushughulikia masuala ya rushwa ya kikanda.”
Kadhalika Mheshimiwa
Majaliwa amesema kuwa Tanzania kwa upande wake, inachukulia mapambano dhidi ya
rushwa kama kipaumbele cha kitaifa na jambo la msingi kwa maendeleo Taifa na
usalama wa Taifa.
“Njia iliyo mbele huenda
ikawa ndefu, lakini tusiwaze kushindwa. Kwa ushirikiano endelevu, maono ya
kimkakati, na utashi wa kisiasa, tunaweza na tunapaswa kujenga ukanda wa SADC
usio na rushwa.”
Mheshimiwa Majaliwa
amewapongeza viongozi hao kwa kuendelea kusimamia mikakati mbalimbali ya kupiga
vita rushwa ikiwemo kuanzishwa kwa mfumo imara ya ufuatiliaji, tathmini na
utoaji wa taarifa SADC. Pamoja na Kielelezo cha Jitihada za Kikanda za
Kupambana na Rushwa.
Kwa upande wake, Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stegomena Tax amesema kuwa Serikali
ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,
inaendelea kusimama imara katika kuendeleza
utawala bora na kuheshimu utawala wa sheria, ambayo ni nguzo kuu katika
mapambano yao ya pamoja dhidi ya rushwa.
“Warsha hii, imekuja
wakati muafaka, ikiwa ni jukwaa la kubadilishana uzoefu bora, kuimarisha
ushirikiano, na kuoanisha juhudi zetu katika kupambana na rushwa kwa ufanisi
zaidi katika ukanda huu.”
Naye, Mwenyekiti wa
Kamati ya Kupambana na Rushwa ya SADC, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa
TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila amesema kuwa kupitia mikakati Miwili ya
Kupambana na Rushwa ya (2018-2022) na (2023-2027), wamefanikiwa kuandaa mtaala
wa Kikanda uliowekwa viwango vya uchunguzi na kinga dhidi ya rushwa, kuandaa
Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Kikanda wa Kupambana na Rushwa pamoja na
Kuandaliwa kwa Tathmini ya Kikanda ya Mapambano Dhidi ya Rushwa.
0 Maoni