Mkurugenzi wa Idara ya Tawala za Mikoa kutoka OR-TAMISEMI Bi. Beatrice
Kimoleta amewataka wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi wa mitaro ya
maji kuzunguka maeneo yao.
Bi. Kilemeta ameyasema hayo alipotembelea banda la Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) kwenye Maonesho ya NaneNane Kitaifa kwenye viwanja
vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema kwamba wapo baadhi ya wananchi hawasafishi mitaro ya maji kwenye
barabara zinazopita kwenye nyumba zao na hivyo maeneo yao kuwa machafu wakati
wote.
“TARURA endeleeni kutoa elimu kwa wananchi wasafishe mitaro inayopita
kwenye nyumba zao,ipo mitaa unakuta kuna barabara nzuri za lami lakini kuna
nyasi nyingi na wengine wana magenge mbele ila uchafu wote wanatupa kwenye
mitaro hiyo na hawasafishi”.
Ameongeza kusema kwamba wananchi wakijenga utamaduni wa kusafisha na
kulinda miundombinu ya barabara inayowazunguka, itadumu kwa muda mrefu.
Aidha, amewapongeza TARURA kwa kazi nzuri wanayoifanya nchini kwa
kuwafungulia barabara wananchi na hivyo kuwarahisha mawasiliano katika maeneo
mengi.
Naye, Bw. Frank Urio Mkazi wa kijiji cha Kimangaro, Kata ya Mwika Kusini Wilaya ya Moshi vijijini
ameipongeza TARURA kwa kuwawezesha kujenga barabara katika kijiji chao Kwa
gharama zao kupitia michango ambapo TARURA imewasaidia ushauri wa kitaalamu
ikiwemo vipimo stahiki vinavyotumika katika ujenzi wa barabara hasa za
vijijini.
Amesema kutokana na kujitolea kwao TARURA imeweza kuipa kipaumbele barabara
hizo kwa kutoa wataalam wao kusimamia ujenzi wa barabara hizo , kukubali
kujenga makalavati ili maji yasiharibu barabara hizo pamoja na kuweka changarawe na hivyo kusaidia nguvu za
wananchi.
Hata hivyo Bw. Urio ametoa wito wa wananchi wa Kimangaro, Kiruweli na
vijiji vingine waliojitolea na kufaidika na barabara hizo wazitunze na
kuhakikisha zinakuwa katika hali ya usafi, kutokutupa takataka na hawaharibu
alama za barabarani ili zidumu kwa muda mrefu.
0 Maoni