Wakala wa Vipimo (WMA) imetoa wito kwa wakulima kufika kwenye banda lao katika Maonesho ya Kilimo, maarufu kama Nane Nane, Uwanja wa Nzuguni, Dodoma ili kupatiwa elimu kuhusiana na matumizi ya vipimo katika sekta ya kilimo ili waweze kunufaika.
Wito huo umetolewa na Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma Bi.
Veronica Simba ambapo amesema WMA itamuelimisha mkulima kuanzia pale anapoanza
kuandaa shamba lake ili apande mazao yake kwa kutumia vipimo sahihi.
“Mkulima anapaswa kuachana utamaduni ule wa zamani ambapo walikuwa
wakipima kwa kutumia miguu, tutamuelimisha mkulima namna gani atumie vipimo
sahihi katika kupanda mazao yake ili apate matokeo chanya yenye tija,” alisema
Bi. Veronica.
Pia, Wakala wa Vipimo tutamuelimisha mkulima namna ambavyo anatakiwa
kuyapima mazao yake pindi anapovuna kwa kutumia mzani ambao umehakikiwa na WMA
ili mkulima asipunjwe na wala asimpumje mnunuzi wakati anapouza mazao yake.
“Mkulima atapata elimu kutoka kwa wataalam wetu ni kwa namna gani atumie
mizani kwa usahihi na mizani hizo ni za aina gani ambazo zitampa mkulima
matokeo stahiki na matokeo chanya,” alisema Bi. Veronica.
Ameeleza kuwa Wakala wa Vipimo pia, huwa wanahakiki mbegu wanazonunua
wakulima ambazo huwa zimefungashwa hivyo mkulima akifika katika banda la WMA
lililopo kwenye Banda Kuu la Wizara ya Viwanda na Biashara atapata elimu namna
wanavyomlinda mkulima.
Pamoja na mambo mengine Bi. Veronica amesema kuwa WMA inaamini kwamba mkulima
wa kisasa anatumia umeme na maji, hivyo wao pia wanahusika na uhakiki wa dira
za maji na mita za umeme ili kumlinda mkulima.
0 Maoni