Waziri Chana azindua Mkakati wa Taifa wa Mikoko

 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. PindiChana, amezielekeza taasisi za Serikali, ikiwemo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), taasisi za utafiti na wadau wa maendeleo kuhakikisha zinatekeleza kwa kasi na kwa ufanisi Mkakati wa Kitaifa wa Usimamizi na Maendeleo ya Mikoko 2025–2035, ili kulinda bioanuwai na kuchochea maendeleo ya uchumi wa buluu nchini.

Akizungumza leo Agosti 5,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uhifadhi wa Mikoko, Waziri Chana amezindua rasmi mkakati huo wa miaka 10, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe wa utekelezaji wa mikakati inayotungwa kwa gharama kubwa bila kuleta matokeo kwa wananchi.

"Mikakati haipaswi kuwa makaratasi yanayohifadhiwa kabatini. Lazima taasisi zetu ziweke bajeti, zishirikishe jamii na zitekeleze kwa vitendo. Mikoko ni maisha ya watu wa pwani," alisema Waziri Chana katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli ya Protea Courtyard.

Amezitaka taasisi zinazohusika, hususan TFS, kuanza mara moja utekelezaji wa mkakati huo kwa kushirikiana na wadau wengine, akitaja kuwa ni pamoja na taasisi za utafiti, Wizara ya Maliasili na Utalii, pamoja na washirika wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Waziri Chana, mikoko ni kinga muhimu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile mmomonyoko wa fukwe, huku pia zikiwa chanzo cha fursa mpya za kiuchumi ikiwemo biashara ya kaboni, utalii wa mazingira, ufugaji wa samaki na nyuki.

“Tunapoitunza mikoko, tunatunza kaboni, tunapambana na tabianchi na tunaboresha maisha ya wananchi,” alisema Waziri huyo.

Mkakati huo unakadiriwa kugharimu Sh bilioni 54.7 na unalenga kuhifadhi na kurejesha asilimia 60 ya mikoko iliyoharibiwa nchini. Takwimu zinaonesha Tanzania ina zaidi ya hekta 158,000 za mikoko, ambapo Delta ya Rufiji pekee inahifadhi takriban nusu ya mikoko yote nchini.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu nchini kutoka TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alisema mkakati huo umeandaliwa kwa ushirikiano na wadau wa mazingira, na kuwa nyenzo muhimu ya kuhakikisha uhifadhi endelevu wa mikoko unafanyika kwa kushirikisha jamii na sekta binafsi.

"Kupitia mkakati huu, tutafanya kazi kwa pamoja na jamii, watafiti, na sekta binafsi kuwekeza katika maeneo ya mikoko kama urithi wa taifa," alisema Prof. Silayo.

Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa ya mazingira akiwemo Mkurugenzi Mkazi wa WWF Tanzania, Dkt. Amani Ngusaru, waliupongeza mkakati huo kwa kuwa na mwelekeo wa kisayansi, jumuishi na unaolenga matokeo ya muda mrefu.

"Serikali imeonesha dhamira ya kweli ya kuhifadhi ardhi oevu na mikoko kama sehemu ya vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi," alisema Dkt. Ngusaru.

Mashirika mengine yaliyoshiriki kutoa mchango wa kitaalamu, kifedha na wa kielimu ni pamoja na Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Hifadhi za Baharini na Maeneo Tengefu (MPRU), Mtandao wa Uhifadhi wa Ukanda wa Pwani (Mwambao), Shirika la EarthLungs, pamoja na Wetlands International.




Chapisha Maoni

0 Maoni