Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA) Abdul-razaq Badru ametembea kijiji cha Msomera kilichopo wilayani
Handeni Mkoani Tanga kujionea uendelezaji wa eneo hilo ambalo linatumika kwa
ajili ya kuwamishia wananchi tarafa ya
Ngorongoro wanaojiandikisha kuhama kwa hiari.
Akiwa na mwenyeji wake mkuu wa wilaya ya Handeni mhe. Salum
Nyamwese,kamishna Badru amesema mamlaka itashirikiana na wizara za kisekta
katika kuhakikisha kijiji hicho kinaendelea kuwa cha mfano kwa kukiwekea
miundombinu yote wezeshi kwa ajili ya wananchi wanaohamia.
“Mheshimiwa mkuu wa wilaya kuna kazi kubwa ambayo serikali
imefanya, tutaendelea kushirikiana katika kuhakikisha kijiji hiki kinakuwa
bora ili wananchi waliohamia na wale
watakaohamia waweze kuishi hapa kwa furaha,”alisema Kamishna Badru.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Handeni mhe. Nyamwese
alisema kuwa kazi mbalimbali za uboreshaji wa miundo mbinu katika kijiji hicho
zinaendelea ikiwa sambamba na ulinzi wa Nyumba ambazo zimeshakamilishwa
kujengwa.
Kijiji cha Msomera kimekuwa ni cha mfano kutokana na
serikali ya awamu ya sita kuamua kuweka miundombinu yote ya msingi ili wananchi
wanaoishi eneo la Ngorongoro waweze kuhamia kupisha shughuli za uhifadhi katika
hifadhi hiyo.
0 Maoni