Taasisi ya Jiolojia na
Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kutoa ushauri na huduma za upimaji
wa sampuli za miamba na madini kwa wananchi mbalimbali wanaofika kutaka kujua
aina za miamba na madini waliokuwanayo.
Aidha, GST imekuja na
vifaa vya utafiti wa miamba na madini iliyo chini ya tabaka ya juu la udongo
ambavyo kitaalam vinaitwa vifaa vya
jiofizikia.
Sambamba na hayo, Wataalamu
kutoka GST wamewashauri wananchi kutumia Maabara ya taasisi hiyo kwa uchunguzi
wa sampuli zao za miamba na madini ili
kubaini wingi na uwepo wa madini ili kuongeza tija na uzalishaji wa madini.
Aidha, Wizara ya Madini
kwa kushirikiana na taasisi zake imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu
masuala mbalimbali ya sekta ya madini kupitia banda lake lililopo katika eneo
la mabanda ya Serikali, banda namba 5.
Kupitia banda hilo,
wananchi wanaelimishwa kuhusu shughuli mbalimbali zinazohusu sekta ya madini
zikiwemo Utafiti wa Madini, Sheria na Kanuni zinazosimamia sekta hiyo, Taratibu
za kisheria za kuendesha shughuli za madini, biashara ya madini pamoja na mbinu
bora na salama za uchimbaji wa madini.
Lengo kuu la utoaji wa
elimu hiyo ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata uelewa sahihi kuhusu namna ya
kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini kwa kuzingatia Sheria na Miongozo
iliyopo, huku wakihimizwa kufanya shughuli hizo kwa njia endelevu, salama na
zenye tija.
Pamoja na mambo mengine,
Wizara inawaalika wananchi wote kutembelea banda hilo ili kujifunza zaidi
kuhusu fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya madini, na namna ya
kuzitumia kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Wizara ya Madini
itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu hii inawafikia
wananchi wengi zaidi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita
chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha na
kuendeleza sekta ya madini nchini.
0 Maoni