Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF),
Prof. Fortunata Makene, amesema kuna haja ya nchi za Global South (nchi za
Kusini) kushirikiana na kubadilishana uzoefu ili kujitegemea kiuchumi na kupata
nafasi kubwa katika utawala wa kimataifa.
Ameyasema hayo leo kwenye mdahalo wa wataalam uliofanyika katika ukumbi
wa ESRF, uliolenga "kubadilishana maarifa" juu ya nafasi ya Global
South duniani.
"Tulianza ushirikiano na Chuo Kikuu cha Kilimo cha China mwaka 2017,
lakini mwaka jana tulisaini mkataba wa uhusiano ili kuendelea kufanya
majadiliano yanayohusisha nchi za Global South," alisema Prof. Makene na
kuongeza:"Tunaona ushirikiano unahitajika kwa sababu mifumo yetu ya
maendeleo ni tofauti kidogo. Ni muhimu tujadili namna gani nchi hizi zinaweza
kushirikiana."
Prof. Makene alibainisha kuwa mdahalo huu umekuja wakati muafaka kutokana
na mabadiliko makubwa ya kimataifa. Alitolea mfano wa hatua za Marekani na
Uingereza za kupunguza misaada kwa nchi nyingi, jambo lililosababisha sintofahamu
na mahangaiko.
"Kama Watanzania na kama Global South, tuna wenzetu wa Kusini
wamepitia changamoto za maendeleo lakini wamefika mbali," alisema.
"Kuna China, Malaysia, Singapore, na Korea Kusini. Tulijinyakua uhuru
pamoja nao lakini wako mbali sana. Tunakosea wapi?"
Aliongeza kuwa tatizo linaweza kuwa linatokana na kujikita zaidi kwenye
mifumo ya maendeleo ya nchi za Magharibi au Kaskazini, ambayo inaweza isiendane
na mazingira halisi ya Watanzania.
Mmoja wa wataalamu katika mdahalo huo alipendekeza kuangalia namna ya
kuweka mfumo wa maendeleo unaomlenga Mtanzania bila kumwondoa sana kutoka
kwenye mazingira yake halisi.
Prof. Makene alishangazwa na hali ya nchi za Global South kuhangaika
misaada inapokatwa, licha ya kuwa na rasilimali nyingi za kutosha. Alisema
Tanzania ina ardhi yenye rutuba na madini mengi, na inaweza kulisha bara zima
la Afrika.
Alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na China, ambapo wataalam kutoka Chuo
Kikuu cha Kilimo cha China wamekuwa Morogoro kwa miaka kumi wakifanya kazi ili
kuleta mbinu mbalimbali za kilimo ambazo ziliwasaidia China kufanikiwa.
"Tumeamua kushare knowledge (kubadilishana maarifa) na wataalam wetu
ili tuweze kujifunza kutoka kwao, na wao wajifunze kutoka kwetu," alisema
Prof. Makene. "Kushirikiana ndiyo njia pekee ya kufikia maendeleo endelevu
na kujitegemea kiuchumi."
Katika madahalo huo Wanazuoni wa Kitanzania na Kichina wamesisitiza
umuhimu wa nchi za Kusini (Global South) kuondokana na utegemezi wa misaada na
badala yake kutumia maarifa na rasilimali zao kujiletea maendeleo.
Wamesema hayo katika mdahalo huo wa tatu wa wataalamu wa China na
Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa ESRF, jijini Dar es Salaam.
Mdahalo huo, ulioshirikisha wanazuoni kutoka ESRF, Chuo Kikuu cha Kilimo
cha China (CAU), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,
ulijikita katika jukumu la Global South katika utawala wa kimataifa.
Profesa Andrea Kifasi na Profesa Samuel Wangwe walihimiza mataifa
kutafuta vyanzo mbadala vya ufadhili wa maendeleo, huku Prof. Wangwe akirejelea
falsafa ya Mwalimu Nyerere ya kujitegemea. Dk. Richard Mbunda alisisitiza
umuhimu wa "utawala wa chakula" (food sovereignty) kwa kuwasaidia
wakulima wadogo na kupunguza utegemezi wa nje.
Profesa Zhang Lei alisisitiza kuwa Global South ina rasilimali nyingi za
kutosha kujenga mifumo yake ya maendeleo na kuhamasisha wananchi wake. Mkutano
huo pia ulionesha mafanikio ya ushirikiano kati ya Tanzania na China, ukitoa
mfano wa mradi wa kilimo wa "Small Technologies, Big Harvests."
unaoendeshwa Morogoro.
0 Maoni