Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewaasa wazalishaji wa Maudhui
Mtandaoni kutotoa taarifa ambazo zitaleta taharuki na machafuko ndani ya nchi
hasa katika kuelekea kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakao
fanyika baadaye mwaka huu.
Hayo yamesemwa jana Agosti 3, 2025
na Meneja Kitengo cha Huduma za Utangazaji, TCRA, Injinia Andrew Kisaka
wakati akiwasilisha makala (mada) katika
mkutano ulioandaliwa na wa Tume Huru ya Uchaguzi nchini (INEC) kwa watoa maudhui mtandaoni, amesema kuwa wakati
wa uchaguzi kuna mazingira ya migawanyiko, mivutano ya kijamii, na upotoshaji
wa hali ya juu hivyo ni muhimu kuepuka kusambaza uvumi, kuripoti kwa umakini, kutopendelea
upande wowote na kukemea lugha za chuki.
Kisaka amewataka wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni nchini kote kuimarisha
maadili yao na kuchukua jukumu muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika
kwa amani kwa kupandisha maudhui yenye tija na kama unaona maudhui yataleta
taharuki ni bora kuachana nayo.
Aidha, Kisaka ametoa mfano wa
Historia ya machafuko ya uchaguzi yaliyotea katika nchi Kenya (2007) na Nigeria (2011), amesema kuwa katika
machafuko hayo zaidi ya watu 800 walipoteza uhai nchini Nigeria mwaka 2011
wakati nchini Kenya zaidi ya watu 1,000 walipoteza uhai na wengine 600,000
kupoteza makazi.
Aidha, amesema kuwa katika
mazingira magumu yenye shinikizo la juu la uchaguzi, vyombo vya habari vinaweza
kujikuta vikichangia machafuko kwa kueneza uvumi au kuchochea upendeleo wa
kisiasa.
Amesema ili kukabiliana na maafa wakati wa uchaguzi na baada kuna
miongozo ya kuripoti ambayo inatatua changamoto hizo.
"Uvumi ndiyo chanzo kikuu cha vurugu hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuchunguza kwa
kina uvumi na kutoa taarifa sahihi haraka iwezekanavyo ili kuzuia mzunguko wa
vurugu za kulipiza kisasi." amesema Mhandisi Kisaka.
Pia amehimiza waandaaji wa Maudhui Mitandaoni wakiwamo Mabloga kukataa
lugha na vichwa vya habari vya kichochezi.
"Msiripoti kila kauli ya uchochezi kutoka kwa wanasiasa, hata kama
kauli hizo zinaonekana kuwa habari kwenu na zenye kuvutia msomaji acha kabisa
ni muhimu kutokuzirudia kwenye vichwa vya habari, " amesema Mhandisi
Kisaka na kuongeza kuwa lugha inayodhalilisha inaweza kuchochea wananchi
kutenda vitendo vya kikatili.
Aidha, amesema kuwa katika kipindi
hiki cha uchaguzi, ni vyema wazalishaji
wa Maudhui Mtandaoni kuchukua tahadhari binafsi
kutoa matangazo ya moja kwa moja
'live' ya mikutano ya kampeni za
wagombea kwa sababu yanaweza leta
machafuko.
"Matangazo ya moja kwa moja 'live'
ya machafuko ya uchaguzi yanatakiwa kufanywa na Waandishi Waandamizi
na wenye
uzoefu na siyo 'One Man Show' kama ilivyo kwa baadhi ya wazalishaji wa
Maudhui Mtandaoni.
Wanaohamasisha chuki na vurugu hawapaswi kupewa nafasi hewani,"
amesema Mhandisi Kisaka.
Aidha, amesema kuwa vyombo vya
habari vinapaswa kuzuia kuonesha picha zinazochochea vurugu na ikiwa
ni lazima, kusimamisha matangazo ya moja kwa moja ili kuzuia hali kuwa
mbaya zaidi.
Maafa na miongozo ya kuripoti katika hali ambapo uchaguzi unafanyika
wakati wa maafa, ni sehemu ya elimu zinazotolewa kwa wazalishaji wa Maudhui Mtandaoni katika
kuhakikisha taifa linavuka salama katika uchaguzi wa mwaka 2025 kama ilivyokuwa
katika chaguzi nyingine.
0 Maoni