Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kupitia Kanda ya
Kaskazini, inaendelea kutumia jukwaa la Maonesho ya Nane Nane 2025
yanayoendelea katika Viwanja vya Nane Nane mkoani Arusha kuwafikia Watanzania
kwa kuwapatia elimu kuhusu uhifadhi, utalii na fursa za uwekezaji katika maeneo
yake ya usimamizi.
Kupitia ushiriki wake ndani ya banda la pamoja la Wizara ya Maliasili na
Utalii, TAWA inatoa taarifa na elimu kwa umma kuhusu vivutio vya utalii
vilivyoko Kanda ya Kaskazini na maeneo mengine nchini, sambamba na fursa za
uwekezaji katika sekta ya uhifadhi. Maonesho hayo yaliyoanza rasmi tarehe 1
Agosti 2025 yamekuwa jukwaa muhimu la kuwasiliana moja kwa moja na wananchi.
Mbali na utoaji wa elimu, TAWA kwa kushirikiana na wadau wake imewavutia
wananchi kwa kuonesha Wanyamapori hai wakiwemo Simba, Fisi na Mamba ambao
wamekuwa kivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mkoa wa
Arusha wanaotembelea banda la Maliasili na Utalii.
Takwimu za awali zinaonesha kuwa kufikia tarehe 3 Agosti 2025, zaidi ya
wananchi 350 wamepokea huduma ya elimu na maelezo kutoka kwa wataalamu wa TAWA.
Kazi ya uelimishaji na uhamasishaji inaendelea hadi kilele cha maonesho hayo
mnamo tarehe 8 Agosti 2025.
TAWA inahimiza wananchi wote kutembelea banda la Maliasili na Utalii ili
kupata taarifa sahihi, kujifunza kuhusu utalii wa ndani, na kufahamu nafasi
walizonazo katika kulinda urithi wa taifa na kuchangamkia fursa za uwekezaji
zinazotolewa.



0 Maoni