Waziri Ridhiwani Apongeza Mafanikio Makubwa Ofisi ya Msajili wa Hazina

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, ameipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa mafanikio makubwa katika kuboresha utendaji wa mashirika ya umma nchini.

Akizungumza Ijumaa, Julai 4, 2025, wakati wa ziara yake katika banda namba 39 (Ukumbi wa Kilimanjaro) kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mhe. Kikwete alisema mageuzi hayo yamechangia mashirika mengi ya umma kujiendesha kwa ufanisi na kutoa mchango mkubwa kwa Serikali.

"Tunaishukuru Ofisi ya Msajili wa Hazina chini ya uongozi imara wa Bw. Nehemiah Mchechu kwa kuwezesha taasisi za umma kuongeza ufanisi wao," alisema Mhe. Kikwete.

Akiweka mkazo juu ya mafanikio hayo, Mhe. Kikwete alieleza kuwa mageuzi hayo ni sehemu ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha utendaji katika sekta ya umma.

"Wote ni mashahidi, tumeona mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika taasisi za umma, hali ambayo haikuwahi kushuhudiwa miaka ya nyuma," alisema.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, mashirika kadhaa ambayo awali yalikuwa yanapata hasara sasa yameimarika kifedha na kuanza kutoa gawio kwa Serikali. Miongoni mwa mashirika hayo ni pamoja na OSHA, ambalo kwa mwaka wa fedha 2024/25 limechangia Shilingi bilioni 10.5 kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.

Mashirika mengine yaliyotajwa kuonesha ufanisi mkubwa ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Akitoa mfano wa mafanikio hayo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw. Sabato Kosuri, alisema ufanisi umeongezeka kwa kiwango kikubwa kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA).

"Kwa mwaka wa fedha uliopita, Mamlaka ya Bandari imeongeza mchango wake kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali kutoka Shilingi bilioni 155.7 mwaka 2023/24 hadi Shilingi bilioni 181 mwaka 2024/25," alisema Bw. Kosuri.

Aidha, matumizi ya kawaida kwa ajili ya uendeshaji wa bandari yamepungua kwa kiasi cha Shilingi bilioni 505.59, ikiwa ni ufanisi wa asilimia 46.

Waziri Kikwete aliihakikishia Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Serikali itaendelea kuiunga mkono katika jitihada zake za kuimarisha taasisi za umma.

“Endeleeni kufanya kazi kwa bidii. Pale ambapo kuna mambo yanayohitaji kubadilishwa katika taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hesabuni mmepata ushirikiano kutoka kwetu,” alisema.

Maonesho ya Sabasaba mwaka huu yamehudhuriwa na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, zikiwa na lengo la kuonesha mafanikio na huduma wanazotoa kwa wananchi, sambamba na kukuza ushirikiano wa kibiashara.




Chapisha Maoni

0 Maoni