Lugha ya kiswahili na
utamaduni wa mtanzania vimeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali
wa kimataifa waliotembelea banda la Tanzania katika Wiki ya utamaduni na
Kiswahili inayoendelea kwenye maonesho ya biashara ya dunia (Expo 2025)
yanayofanyika Osaka.
Viongozi waandamizi
wa mataifa mbalimbali, wametembelea banda hilo ikiwemo Naibu Spika wa Baraza la
Wawakilishi la Japani, Bw. Koichiro Gemba, Mfalme wa Lesotho, Mhe. Letsie III
na Mhe. Prudence Sebahizi, Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda.
Viongozi hao
wameonesha kuvutiwa kwa kiasi kikubwa na lugha ya Kiswahili na Utamaduni kupata
nafasi katika Maonesho hayo ya Dunia yenye hadhi kubwa.
Akizungumza wakati
alipotembelea banda hilo Mhe. Sebahizi alieleza kufurahishwa na namna lugha ya
Kiswahili ilivyopewa nafasi katika maonesho hayo ya dunia na kudai Kiswahili
kinaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuwaunganisha Waafrika katika juhudi zao za
kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Akizungumza na
maofisa wa taasisi za Tanzania zinazoshiriki katika maonesho hayo, ikiwemo
Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar
(SUZA), Mhe. Sebahizi amesema kuwa lugha ya kiswahili inakidhi kwa matumizi
miongoni mwa Waafrika.
Viongozi hao pia
walipata fursa ya kujionea vivutio vya kitamaduni kama vile mavazi ya jadi,
sanaa za mikono, bidhaa za kipekee kama kahawa ya Kilimanjaro, Madini ya
Tanzanite, viungo vya asili vya Zanzibar na machapisho mbalimbali ya Kiswahili
huku Kamusi Kuu ya Kiswahili kutoka BAKITA ikiwavutia wengi.
Ushiriki huu wa
Tanzania katika maonesho hayo ambayo kwa upande wa Tanzania yanaratibiwa na
TanTrade, ni sehemu ya juhudi endelevu za kuitangaza lugha ya Kiswahili kama
urithi wa Afrika na dunia, sambamba na utamaduni wake tajiri, ili kuimarisha
uhusiano ya kimataifa na kuvutia wawekezaji, watalii na washirika wa maendeleo
kupitia nguvu ya lugha na utambulisho wa kitaifa.
Kilele cha wiki hii
ya Utamaduni na Kiswahili katika maonesho hayo kitafanyika tarehe 7 mwezi wa 7,
ambapo kwa kawaida huwa ni Maadhimisho ya Siku Kiswahili Duniani (MASIKIDU),
ambapo kutakuwa na utoaji wa vyeti na tuzo mbalimbali kwa wadau walioshiriki
kwa hali na mali kukikuza, kukieneza, na kukiendeleza Kiswahili nchini Japani.
0 Maoni