Jukwaa la Wahariri Tanzania
(TEF) limempongeza Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ndugu
Ernest Sungura, kwa kuchaguliwa kushika nafasi mbili muhimu za kimataifa katika
sekta ya habari.
Sungura ameteuliwa kuwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabaraza ya Habari Duniani (WAPC), pia Makamu
Mwenyekiti wa Mabaraza ya Habari ya Afrika Mashariki (EAPC), hatua ambayo TEF
imeielezea kuwa ni heshima kwa taifa na tasnia ya habari kwa ujumla.
Akitoa pongezi hizo leo kupitia
taarifa kwa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alisema kuwa
uteuzi huo si tu unamtambulisha Sungura kimataifa, bali pia unaonesha jinsi
Tanzania inavyoendelea kutoa mchango mkubwa katika kukuza na kulinda taaluma ya
habari duniani.
“TEF inatambua juhudi na
uongozi mahiri wa Ndugu Sungura, ambao umejenga misingi imara ya ushirikiano wa
kikanda na kimataifa kupitia Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA),
na sasa ameendelea kupanda hadi ngazi ya WAPC,” alisema Balile.
Aliongeza kuwa mchango wa
Sungura katika kuimarisha mazingira wezeshi ya uhuru wa habari, uwajibikaji, na
weledi katika sekta ya habari umekuwa wa kuigwa, na sasa dunia inatambua juhudi
hizo.
“Tunamtakia kila la heri
katika majukumu yake mapya ya kimataifa, na tunamhakikishia kuwa TEF itaendelea
kushirikiana naye kwa karibu kwa maendeleo ya tasnia ya habari nchini na
duniani kote,” alisema Balile.
Uteuzi huo unakuja wakati
ambapo sekta ya habari inaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwamo
za kiuchumi, huku mchango wa viongozi kama Sungura ukihitajika zaidi katika
kuimarisha maadili, uwazi na uhuru wa vyombo vya habari.
0 Maoni