Waziri wa Madini,
Mhe. Anthony Mavunde (Mb) abainisha kuwa mradi wa kimkakati wa uchimbaji
wa madini ya Urani kuanza hivi karibuni baada ya kukamilika kwa ujenzi wa
kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa madini hayo.
Mhe. Mavunde ameyasema hayo jana
tarehe 18 Julai, 2025 Wilayani Namtumbo alipofanya ziara ya kutembelea na
kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo unaokadiriwa kugharimu zaidi ya Tsh
3.06 Trilioni unaotekelezwa na Kampuni
ya Mantra Tanzania Limited.
"Moja kati ya
vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia
S.Hassan kwenye sekta ya madini ni suala la uongezaji thamani madini ndani ya
nchi yetu, na Mhe. Rais ametupa maelekezo mahsusi Wizara kusimamia hili."
"Kuanza kwa mradi
huu ambao unahusisha pia ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani madini ya urani
unadhihirisha utekelezaji wa azma ya Serikali kwa vitendo. Katika hili, sisi
Wizara ya Madini tutaendelea kusimamia kikamilifu ili kunufaisha Nchi yetu,"
alieleza Mhe. Mavunde.
Uwepo wa mashapo
yanakadiriwa kufikia tani milioni 139 na kufanya maisha ya mgodi kukadiliwa
kuwa miaka 22, kunaifanya Tanzania kuingia kwenye ramani ya dunia na kuwa
miongoni mwa Nchi 10 zinazozalisha madini ya Urani kwa wingi duniani.
Akieleza baadhi ya manufaa
ya mradi huo, Waziri Mavunde alisema ukiachana na ajira za moja kwa moja zaidi
ya 4000, ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 100,000 Kampuni ya Mantra
imeanza majadiliano na serikali ili kuhakikisha inajenga mtambo wa kuzalisha
umeme kwa kutumia Urani itakayochimbwa mgodini hapo.
Aidha, Mhe. Mavunde
alitanabaisha kuwa pamoja na manufaa makubwa kwa Nchi kupitia mapato, mradi huo
unakwenda kubadilisha taswira ya Namtumbo kwani unakwenda kugusa maisha ya
wananchi wengi wanaozunguka mradi.
Awali, akitoa maelezo ya
mradi, Meneja wa Uendelezaji Mradi kutoka Kampuni ya Mantra, Bw. Majani Moremi
aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kampuni kulikowezesha
kufanikisha kuanza kwa mradi huo, na kuahidi mradi unakwenda kuleta tija na
mafanikio tarajiwa kwa Nchi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Ruvuma, Mh. Kanali Ahmed Abbas alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa
kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji nchini yaliyopelekea mradi huo kutekelezwa
Mkoani Ruvuma, na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kampuni ya Mantra
muda wote ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa manufaa ya Nchi na
wananchi wa Namtumbo.
0 Maoni