Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kimetangaza kusogeza mbele tarehe ya uteuzi wa mwisho wa wagombea wake wa
nafasi za Ubunge na Udiwani kutoka Julai 19 hadi Julai 28, 2025.
Akizungumza na waandishi
wa habari leo Julai 19, 2025, jijini Dodoma, Katibu wa Itikadi, Uenezi na
Mafunzo wa chama hicho, Ndg. Amos Makalla amesema kuwa mchakato wa ndani
unaendelea vizuri huku uchambuzi wa majina ya wagombea ukifanyika kwa umakini
mkubwa.
“Maandalizi ya mchakato
wa uchaguzi ndani ya CCM yanaendelea vizuri. Kikao cha mwisho cha uteuzi wa
wagombea sasa kimepangwa kufanyika Julai 28, 2025 hapa Dodoma, badala ya leo
Julai 19, 2025. Wagombea ni wengi sana, kazi ya kuchambua ni kubwa, na sisi
tunataka tufanye kwa umakini,” alisema Makalla.
Amesema chama hicho
kimeongeza muda wa mchakato huo ili kuhakikisha kuwa kila hatua ya uchambuzi wa
wagombea inafanyika kwa makini na kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na chama, “Wagombea
wa relax (watulie) wakati tunaendelea na mchakato.”
Hatua hiyo ni sehemu ya
maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu,
ambapo CCM kama chama tawala kinaendelea na mchakato wa kuwapata wagombea wake
watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Uamuzi huo unakuja wakati
ambapo macho ya wanachama na wananchi kwa ujumla yameelekezwa kwa CCM,
wakisubiri kwa hamu majina ya watakaochuana katika kinyang’anyiro cha uchaguzi
mkuu wa mwaka huu.
0 Maoni