Mfanyabiashara maarufu
nchini, Bw. Rostam Azizi, ametoa wito kwa Serikali kuwekeza kwa makusudi katika
rasilimali watu, hususan vijana, ili kuiwezesha Tanzania kupiga hatua kubwa za
maendeleo katika karne ya 21.
Akitoa maoni yake jana katika hafla ya uzinduzi wa Dira 2050, Bw. Azizi alisema hatua ya kwanza ni kuanzisha
Mfuko wa Maendeleo ya Vipaji wenye bajeti ya takriban Dola za Kimarekani
milioni 70 kila mwaka kwa kipindi cha miaka kadhaa, ili kuwajengea uwezo vijana
takribani 1,000 katika nyanja za kimkakati kama vile Uhandisi, Akili Bandia
(AI), Sayansi ya Takwimu, Fedha, pamoja na kozi nyingine zitakazotambuliwa
kulingana na mahitaji ya taifa.
“Kupitia mpango huu,
tutawapeleka vijana wetu kusoma katika vyuo bora duniani kama vile vilivyoko
Marekani, Uingereza na China, kisha warejee kuja kuhudumu katika taasisi za
serikali kwa mkataba maalum,” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa
mpango huo si wa masomo pekee bali ni uwekezaji wa kimkakati katika wasanifu wa
mwelekeo mpya wa taifa kama ulivyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa
2050.
Vyuo vya Ndani Navyo Vipewe Kipaumbele
Hata hivyo, Bw. Azizi
alisisitiza kuwa nchi haiwezi kusubiri mpaka vijana walioko nje warejee ndipo
hatua zichukuliwe. Alitaka vyuo vya ndani viimarishwe, mitaala iboreshwe,
utafiti uongezwe, na mfumo wa elimu uendane na mahitaji ya sasa ya kiuchumi.
“Tunapaswa kuhakikisha
vyuo vyetu vina uwezo wa kuzalisha wataalamu wa viwango vya kimataifa. Hatuna
budi kuboresha mfumo wetu wa elimu kutoka ndani,” alisema.
Viongozi Pia Wapate Mafunzo ya Kimataifa
Katika hoja nyingine, Bw.
Azizi alipendekeza kuwa viongozi waliopo katika taasisi mbalimbali za umma
wapewe fursa ya kushiriki katika programu za uongozi za kimataifa, ili
kuwajengea uwezo wa kuongoza katika mazingira mapya.
“Hii itawasaidia
kuvitumia vizuri vipaji vipya vitakavyoibuka,” aliongeza.
Balozi Watambue Watanzania Wenye Ujuzi Ughaibuni
Kama hatua ya dharura,
aliishauri Serikali kupitia balozi zake kuwatambua na kuwarudisha nyumbani
Watanzania walioko nje wanaosomea au kufanya kazi katika nyanja muhimu, ili
taifa linufaike na maarifa yao.
“Kwa bahati nzuri tuna
Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Mahmood Thabit, ambaye anaamini sana katika
kutumia diplomasia kwa maendeleo ya uchumi wa nchi – mimi humuita Waziri wa
Diplomasi ya Uchumi,” alisema kwa msisitizo.
Sekta Binafsi na Viwanda Vilindwe
Katika hitimisho lake,
Bw. Azizi alisisitiza umuhimu wa Serikali kuilinda sekta binafsi ya ndani, hasa
viwanda, ikiwa taifa linakusudia kufikia uchumi wa dola trilioni moja.
“Tunakushukuru Mheshimiwa
Rais kwa jitihada zako za kuwavutia wawekezaji wa nje, lakini mwisho wa siku
Watanzania ndiyo watakaolijenga taifa lao. Tunapaswa kuwawekea mazingira rafiki
na ya ulinzi wawekezaji wa ndani,” alisema.
Alionya kuwa hakuna nchi
duniani iliyoweza kufanikisha mapinduzi ya viwanda bila kulinda viwanda vyake
vya ndani.
“Serikali izingatie hili
tunapojiandaa kutekeleza Dira 2050,” alihitimisha.
0 Maoni