Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amemkabidhi tuzo ya umahiri Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Nishati, Bi. Neema Chalila
Mbuja, kutokana na mchango wake mkubwa katika sekta ya mawasiliano wakati wa
Maonesho ya Dunia ya Biashara ya Osaka, Japan.
Makabidhiano hayo
yalifanyika jana Julai 13, 2025, wakati wa kilele cha Maonesho ya 49 ya
Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, yaliyofanyika
katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Mhe. Majaliwa alimtaja Bi. Mbuja kuwa ni miongoni mwa watumishi wa umma
waliotoa mchango wa kipekee katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia
mawasiliano ya kisasa, hasa kwenye maonesho ya Osaka Expo 2025.
“Bi. Mbuja ameonyesha
weledi mkubwa katika kuwasilisha na kutangaza fursa za Tanzania kwenye jukwaa
la kimataifa. Amefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi yetu na Wizara ya Nishati
kwa ujumla,” alisema Majaliwa.
Kwa upande wake, Bi.
Mbuja alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutambua juhudi zake na kutoa tuzo hiyo,
ambayo ilitolewa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE).
Aliahidi kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia Wizara ya Nishati katika
majukwaa mbalimbali ya kimataifa.
Tuzo hiyo ni sehemu ya
jitihada za Serikali kutambua na kuthamini watumishi wa umma wanaofanya kazi
kwa weledi na uzalendo katika kuiwakilisha vyema Tanzania nje ya mipaka.
0 Maoni