WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade)
kuendeleza juhudi za kutafuta masoko ya nje ili kuongeza mauzo yatakayowezesha
nchi kupata fedha za Kigeni.
Amesema kuwa TanTrade
inapaswa kufanya tafiti za uhakika na uchambuzi wa masoko ambayo bidhaa za
Tanzania zinaweza kuuzwa na kutoa taarifa hizo kwa wafanyabiashara kote nchini.
Ametoa agizo hilo leo jana
Jumapili, Julai 13, 2025, alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
ufungaji wa Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar-es-Salaam.
“Masoko yamekuwa ya
ushindani sana siku hizi, nilipotaja Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA),
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) nilikuwa nataka kuwaambia kwamba leo hii tunapotaka kufanya uchambuzi wa
masoko yetu, hayo ndio maeneo ya kufanya biashara, TanTrade fanyeni tafiti za
uhakika na uchambuzi wa kina.”
Aidha, Mheshimiwa
Majaliwa ametoa wito kwa wazalishaji wote nchini kuweka mkakati wa kuongeza
uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa ambazo zina mahitaji makubwa katika masoko
ndani na nje ya nchi. “Maonesho haya ya 49 ya biashara yanapaswa kuwapa mwanga
wa bidhaa gani zina mahitaji makubwa ili muweze kuongeza uzalishaji tunahitaji
kupanua wigo wa masoko kwenye mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.”
Kadhalika, amewataka
Wazalishaji hao kuzalisha bidhaa zenye ubora mkubwa ili watumiaji waweze
kuridhika ubora wake na ziweze kumudu ushindani wa kimataifa. “Pamoja na hayo
msisahau kutumia ile haki ha nembo ya Tanzania ambayo ni alama yetu ya Taifa
letu, kila bidhaa unayoizalisha hakikisha pale chini umeandika made in
Tanzania, hiyo ndiyo nembo yetu ya Taifa.”
Pia Mheshimiwa Majaliwa
amezitaka taasisi zote zinazosimamia Biashara na Uwekezaji, Tanzania Bara na
Zanzibar, zihakikishe zinaondoa urasimu na kuwezesha Biashara zaidi badala ya
kuwa kikwazo.
Katika hatua nyingine,
Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia washiriki wa maonesho hayo muwa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar zitaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji zaidi katika maeneo ya
kimkakati ili kuchangia kikamilifu katika pato la taifa na kunufaisha wananchi
wetu.
Kwa Upande wake, Waziri
wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo katika kipindi cha siku 16 cha
maonesho hayo, watu zaidi ya milioni 2.4 wameweza kushiriki katika shughuli
mbalimbali za maonesho hayo ya kimaitaifa ya biashara.
Pia ameongeza kuwa
kupitia nembo ya Made in Tanzania, itaiwezesha nchi kuuza biadhaa zikiwa na
nembo ya Taifa. “Hii ni fahari kubwa sana kwetu sisi watanzania.”
0 Maoni