Mwenge wa Uhuru wakagua miradi ya bilioni 84 Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu, amesema Mwenge wa Uhuru umekimbizwa kwa umbali wa kilomita 895 katika mkoa huo na kukagua jumla ya miradi 52 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 84.

Mhe. Babu alitoa taarifa hiyo leo Julai 5, 2025 wakati wa hafla ya makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kwa Mkoa wa Arusha, iliyofanyika katika kijiji cha Kingori, kata ya Malula, wilayani Arumeru.

Amesema kuwa katika ziara hiyo ya Mwenge, miradi 22 ilizinduliwa rasmi, 20 iliwekewa mawe ya msingi huku mingine 10 ikitembelewa na kukaguliwa. Kwa mujibu wake, miradi yote hiyo imeridhiwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa.

Ameongeza kuwa Mwenge huo pia ulipitia miradi tisa ya kijamii ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano na ushirikiano baina ya sekta binafsi na Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro katika kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa jumla ya mitungi 370 ya gesi safi ya kupikia imetolewa kwa wananchi wa maeneo mbalimbali, ikiwa na thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 18.4, kama sehemu ya jitihada za kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Bw. Ismail Ali Ussi, alipongeza utekelezaji wa miradi hiyo, akisema imefanyika kwa ubunifu, tija na ufanisi mkubwa na inaakisi thamani halisi ya uwekezaji wa fedha za umma.

“Nimevutiwa na utendaji kazi wa Wakuu wa Wilaya katika Mkoa huu. Kama ningekuwa na mamlaka ya ushauri, ningeshauri wasiondoke hapa. Waendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kusimamia maendeleo ya wananchi,” alisema Ussi.

Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuendelea na mbio zake mkoani Arusha, ambapo utazindua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyo desturi ya mbio hizo zinazobeba ujumbe wa kitaifa kila mwaka.



Chapisha Maoni

0 Maoni