Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewapongeza wakulima nchini kwa
jitihada zao za kuzalisha mazao kwa wingi na hivyo kusaidia nchi kuwa na usalama wa chakula ikiwa ni pamoja na kuwezesha sekta ya kilimo
kuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.
Dkt. Biteko ametoa
pongezi hizo Julai 5, 2025 jijini Dodoma wakati akifunga Kongamano la Siku ya
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani.
“Leo sekta ya kilimo
ina mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu, tunazungumza mchango wa GDP wa
asilimia 26, tunazungumza mazao ambayo yanatupa
usalama wa chakula katika nchi yetu, nchi zingine zinahangaika kupata
chakula sisi watu wetu wana uhakikia wa kupata chakula mitaani kwa sababu wakulima
wamewezeshwa kufanya biashara ya kilimo, ” amesema Dkt. Biteko
Amebainisha kuwa
takwimu zinaonesha utendaji wa vyama vya
ushirika umeendelea kuimarika kila
wakati mauzo ya nje yameongezeka.
Ambapo kwa mwaka 2024/2025 jumla ya vyama vya ushirika 1,084 viliuza kahawa na
tumbaku moja kwa moja nje ya nchi kiasi cha Dola za Marekani 344,800,000
ikilinganishwa na Dola za Marekani 325,500,000 kwa mwaka 2023/2024 sawa na
ongezeko la Dola za Marekani 19,300,000.
Dkt. Biteko
amefafanua kuwa Vyama vilivyopata Hati safi ya Ukaguzi kutoka Shirika la
Ukaguzi la Vyama vya Ushirika (COASCO) vimeongezeka kutoka vyama 339 mwaka
2021/2022 hadi kufikia vyama 631 mwaka 2023/2024 sawa na ongezeko la vyama 292
ambayo ni asilimia 86.13.
Aidha, Vyama
vilivyopata Hati isiyoridhisha vimepungua kutoka Vyama 1,198 mwaka 2021/2022
hadi kufikia Vyama 263 mwaka 2023/2024 sawa na upungufu wa vyama 935 ambayo ni
asilimia 78.
Ametoa rai kwa Vyama
kuwawezesha wanawake kwa kuweka mikakati mbalimbali ili idadi ya Vyama vya
Ushirika vya Wanawake iongezeke kutoka Vyama 50 vilivyopo sasa.
Licha ya mafanikio
hayo katika sekta ya kilimo, Dkt. Biteko ameziagiza Wizara za Fedha na Kilimo
kupatia ufumbuzi masuala ya bei ya mazao ya wakulima, pembejeo na mahitaji ya
msingi ya wakulima ili kuendelea kufanya kilimo chenye tija.
“Serikali ya awamu ya Sita inatambua kwamba
Ushirika ni nyenzo muhimu ya kuwasaidia wananchi katika kuunganisha nguvu zao
na kujiendeleza kiuchumi. Hivyo, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi na
jitihada zote zenye lengo la kuhakikisha kuwa Vyama vya Ushirika vinasonga
mbele kiuchumi na kijamii, ” amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa Vyama
vya Ushirika vimekuwa na mchango mkubwa katika kujenga uchumi wa nchi ndio
sababu Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan ameipa msukumo mkubwa sekta ya kilimo. Pia amempongeza Waziri wa Kilimo,
Mhe. Hussein Bashe kwa kuhakikisha sekta hiyo inatimiza maoni ya Rais Samia ya
kuwainua wakulima kiuchumi na kukuza uchumi wa nchi.
Vilevile, amempongeza
Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege kwa
kuwasema wakulima nchini na hivyo kuboresha
utendaji kazi wa Vyama vya Ushirika huku akivitaka Vyama hivyo kuwa na
viwanda vya uchakataji wa mazao ili
kuongeza thamani ya bidhaa na kuongeza wigo wa masoko.
Naye, Waziri wa
Kilimo, Hussein Bashe amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
jitihada mbalimbali za kuboresha sekta
ya kilimo nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti za Wizara ya Kilimo, kutoa
zuruku za mazao na kuanzisha kwa Taasisi
mbalimbali ikiwemo COPRA zinazolenga kutetea maslahi ya wakulima nchini.
Aidha, Mhe. Bashe
amebainisha kuwa utekelezaji wa miradi ya Serikali katika maeneo ya vijijini
kama vile uwepo wa umeme katika vijiji vyote nchini na barabara unachochea
maendeleo vijijii na hivyo hutoa fursa kwa wakulima kuanzisha mashine za
uchakataji mafuta mfano ya alizeti na kusafirisha mazao yao.
Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa mkoa huo sasa una Vyama vya
Ushirika 244 na kwa sasa wananchi wamejua umuhimu wa vyama hivyo hususan
lengo namba saba la kuvitaka kushirikiana na jamii.
Akitoa taarifa ya
miaka mitatu kuanzia mwaka 2022/23 hadi 2024/25 ya hali ya Vyama vya Ushirika
nchini, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Benson Ndiege ametaja
mafanikio kadhaa yaliyopatika ikiwa ni pamoja na kuanzisha Benki ya Ushirika
katika mikoa minne nchini.
Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho
la Vyama vya Ushirika (TFC), Bw. Tito Haule amesema kuwa Maadhimisho hayo kwa
mwaka 2025 wanaushirika nchini wanaungana na wadau wengine duniani hivyo
kufanya kuwa Maadhimisho ya 102 tangu kuanzishwa.
Bw. Haule ametaja
baadhi ya malengo ya mwaka wa Ushirika 2025 kuwa ni pamoja na kutoa fursa kwa
Vyama Vya Ushirika kuonesha bidhaa zao kwa jamii na kuhabarisha umma juu ya
mchango wa Vyama hivyo na kuhimiza uwepo wa sera na desturi.
Aidha, amesema baadhi
ya mafanikio ya Vyama Vya Ushirika nchini ni ongezeko la idadi ya wanachama
kutoka milioni 6.9 mwaka 2021/22 hadi kufikia milioni 10, kuongeza ajira
za kudumu na mikataba kwa vijana na kuchangia pato la kodi kwa Serikali hadi
shilingi bilioni 9.5 mwaka 2020/22 na
shilingi bilioni 12.5 mwaka 2023.
Pia, ameishukuru
Serikali kwa kuongeza mtaji wa shilingi bilioni 5 katika Benki ya Ushirika na
kuimarisha Vyama Vya Ushirika kwa kuongeza matumizi ya TEHAMA.
Na. Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni