WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa ameziagiza Mamlaka za Mikoa na Wilaya kufanya kaguzi za mara kwa mara
katika maeneo yaliyohifadhiwa, vyanzo vya maji na mito ili kudhibiti vitendo
vya uharibifu wa mazingira.
Ametoa agizo hilo leo
(Jumamosi Julai 05, 2025) aliposhiriki katika mbio za Great Ruaha Marathon
(GRUMA 2025) zilizoanzia na kuishia kwenye eneo la Ibuguziwa, ndani ya Hifadhi
ya Taifa ya Ruaha, mkoani Iringa.
“Wekeni utaratibu
mzuri wa matumizi ya vyanzo hivyo, tunataka kuona mikondo yote ya maji
inayokwenda kulisha mto mkuu, inahifadhiwa ili tupate maji mengi na yaweze
kuchangia kwenye shughuli za kimaendeleo, mto Ruaha Mkuu unapeleka maji katika
bwawa letu la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere.”
Mheshimiwa Majaliwa
ameziagiza mamlaka hizo zibainishe vyanzo muhimu vya maji vilivyopo kwenye
maeneo yao na kuweka utaratibu maalum na wawazi juu ya namna ya kuhifadhi
vyanzo hivyo ili viweze kuzalisha maji ya kutosha. “Mimi ninawasihi wekeni
Sheria ndogo zinazodhibiti uharibifu na kutambua vyanzo hivyo ni muhimu katika
maeneo yenu”.
Kadhalika, Mheshimiwa
Waziri Mkuu ameagiza kusimamiwa kwa mipango ya matumizi bora ya ardhi kuanzia
ngazi ya vijiji. “Sambamba na kuhakikisha elimu ya uhifadhi, upandaji miti na
ajenda ya utunzaji wa mazingira inakuwa ya kudumu kuanzia vitongojini mpaka
vijijini.”
Pia, Mheshimiwa
Majaliwa amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za
kuhakikisha anaisimamia sekta ya utalii ili iweze kuwa na tija na kuchangia
katika pato la Taifa.
Mkuu wa Mkoa wa
Iringa Heri James amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia
utekelezaji wa ahadi zake zinazolenga kukuza sekta ya utalii katika ukanda wa
kusini. “Baadhi ya mambo ambayo anayafanya na ni ishara ya kukuza utalii nk
pamoja na kukamilisha uwanja wa ndege wa Iringa, ujenzi wa barabara kutoka
Iringa hadi Msembe, ujenzi hosteli za wageni ndani na nje ya hifadhi, ama kwa
hakika ameamua kuongeza hadhi ya utalii kwenye ukanda huu.”
Naye, Kamishna wa
Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA (T) Musa Nassoro
Kuji, amesema kuwa ujio wa The Great Ruaha Marathon umekuwa baraka kubwa katika
sekta ya utalii ambapo imesaidia kufungua utalii kwa ukanda wa kusini.
“tunataka kuona marathon hii iwe kubwa na ya kimataifa, tangu tumeanza marathon
hii imesaidia kuongeza idadi ya watalii kwenye ukanda wa kusini, tunataka
watalii waje na dunia itutambue kupitia marathon hii.”
Aidha, ameongeza kuwa Shirika hilo litaendelea
kutunza maliasili zilizopo nchini ili kuvirithisha kwa vijazi vijavyo.
Kwa upande wake,
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP),
Shigeki Komatsubara amesema kuwa hizi sio mbio tu bali ni harakati za kulinda
mto Ruaha Mkuu ambao ni muhimu kwa ajili ya ustawi wa binadamu, wanyamapori na
mfumo mzima wa ikolojia “Leo sio tu tunakimbia kwa ajili ya mazoezi bali kwa
uhifadhi na uelewa.”
0 Maoni