Misitu Honey Yatikisa Sabasaba, Wageni Wafurika Kuionja na Kununua Asali Bora ya TFS

Katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam, bidhaa moja imeibuka kuwa kivutio kinachowakutanisha wageni wa ndani na nje ya nchi kwenye banda la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) — nayo si nyingine bali ni Asali Bora ya Misitu Honey.

Wakazi na wageni kutoka mataifa mbalimbali wamefurika kwenye duka la TFS lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, wakijionea na kuonja bure ladha halisi ya asali safi inayozalishwa kutoka misitu inayosimamiwa kwa uangalizi mkubwa.

Mhifadhi Subira Matumbwa, akizungumza na mwandishi wetu na wageni waliotembelea banda hilo, amesema kuwa idadi kubwa ya watu wamevutiwa na ladha safi, rangi halisi na ubora wa Misitu Honey unaotokana na mnyororo wa uzalishaji wa kitaalamu na uhifadhi endelevu wa misitu.

“Watu wengi wamefurahia kuonja bure na kununua. Wengi wanapongeza radha safi isiyo na kemikali, na sifa nyingine kubwa ni kuwa asali hii ina virutubisho vya asili vinavyosaidia kuongeza kinga ya mwili, kuimarisha afya na haina viambato bandia,” amesema Mhifadhi Matumbwa.

Mbali na asali safi, banda hilo pia limepamba maonesho kwa bidhaa za asali zilizoongezewa thamani kama asali yenye mchanganyiko wa ndizi, mdalasini na hatta alizeti, huku asali ya alimondi ikiwa kivutio kipya kabisa. Bidhaa hizo zinapatikana kwa ujazo unaokidhi mahitaji ya kila mteja kuanzia gramu 500 hadi kilo 5.

Wananchi wametakiwa kutumia fursa hii kufika Sabasaba, kutembelea banda la TFS na kujipatia asali bora ya Misitu Honey kwa manufaa ya afya zao na kuongeza kipato kwa kuchangia sekta ya misitu endelevu.

Wito kwa wananchi “Tunawahamasisha Watanzania wajitokeze kwa wingi Sabasaba. Waje waonjee bure, wanunue na waendelee kutumia Misitu Honey, asali bora, salama na yenye manufaa kwa afya zao na familia zao,” amehimiza Mhifadhi Matumbwa.




Chapisha Maoni

0 Maoni