Mhifadhi mstaafu avutiwa na mapinduzi makubwa ya TFS kwenye Sabasaba

 

Mhifadhi mstaafu aliyewahi kuwa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Ugani na Uenezi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Charles Ngatigwa, leo Juni 3, 2025, ameonesha kufurahishwa na hatua kubwa za maboresho zinazofanywa na TFS katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Ngatigwa, ambaye alitembelea banda la TFS mapema leo akiwa ameongozana na wajukuu zake, amesema ameshangazwa na kufurahishwa kuona mabadiliko makubwa kuanzia muonekano wa banda hadi huduma za ubunifu zinazotolewa, ambazo zimeendelea kuhamasisha wananchi wengi zaidi kutembelea na kujifunza.

“Kweli nimeona mapinduzi makubwa sana. Kipindi nikiwa kwenye utumishi tulikuwa na changamoto nyingi za uhamasishaji na elimu, lakini leo hii nimejionea mwenyewe jinsi TFS inavyotumia fursa ya Sabasaba kufundisha na kutoa huduma kwa vitendo. Hii ni hatua kubwa na ya kupongezwa,” amesema Ngatigwa.

Wajukuu zake walivutiwa zaidi na shamba darasa la ufugaji nyuki lililoandaliwa na TFS ndani ya banda hilo, na kufikia hatua ya kuomba wafundishwe hatua kwa hatua jinsi ya kufuga nyuki na kupata mazao yake.

Mhifadhi anayeshughulikia Dawati la Nyuki TFS, Said Abubakar, alitumia muda huo kuwapa mafunzo ya moja kwa moja kuhusu mnyororo mzima wa thamani wa ufugaji nyuki kuanzia maandalizi ya mizinga, tabia za nyuki, ukusanyaji wa asali na bidhaa zingine zinazotokana na nyuki.

Mbali na kujifunza, vijana hao pia walipata fursa ya kuonja asali safi na kushuhudia jinsi nyuki wanavyofanya kazi. Aidha, kama sehemu ya huduma maalum ya api-therapy inayotolewa bandani hapo, waliruhusiwa kudungwa na nyuki kwa lengo la kujionea manufaa ya tiba hiyo asilia inayozidi kupata umaarufu duniani.

Wote walikiri kufurahia huduma hiyo na kuahidi kurudi tena kujifunza zaidi na kufuatilia fursa za kuanzisha miradi midogo ya nyuki majumbani mwao.

Ngatigwa ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa ya Sabasaba kutembelea banda la TFS ili kujifunza masuala mbalimbali yahusuyo uhifadhi, fursa za uwekezaji kwenye sekta ya misitu na nyuki, pamoja na huduma nyingine za kitaalamu.

“Mtu yeyote anaweza kupata fursa ya kutundika mizinga kwenye misitu iliyohifadhiwa bure kabisa na kupewa elimu ya ufugaji na wataalamu wa TFS bila gharama yoyote. Hii ni hazina kubwa, wananchi wengi hawajui,” amesema Ngatigwa.

Aidha, amewahimiza wananchi wanaopenda kutumia asali kama tiba lishe kuhakikisha wanapita katika duka maalum la Misitu Honey Shop lililopo ndani ya banda la TFS ili kupata asali safi, salama na yenye viwango vya ubora vilivyohakikishwa.

TFS itaendelea kutoa huduma na mafunzo hayo kwa wananchi katika viwanja vya Sabasaba hadi Juni 13, 2025.




Chapisha Maoni

0 Maoni