Hali ya upatikanaji
wa huduma ya majisafi imeendelea kuimarika katika maneno mbalimbali ya Mkoa wa
Dar es Salaam na Pwani mara baada ya kukamilika kwa matengenezo kinga ya
miundombinu ya umeme yaliyodumu kwa Saa 10 na kusababisha kuzimwa kwa Mtambo wa
Ruvu Juu na Ruvu Chini.
Mamlaka ya Majisafi
na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeingia mtaani kufuatilia
upatikanaji na uimarikaji wa huduma, huku wakitoa wito kwa Mamlaka kuendelea
kuboresha huduma kwa kutoa muda mrefu wa kuhifadhi maji pindi wanapoamua
kufanya matengenezo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa
Kambangwa, Kata ya Mwananyamala Ndugu Mkakata Abdul ameeleza kuwa wananchi
walipata adha za kukosa huduma kwa siku mbili (Julai 1 na 2, 2025 ) lakini
kwasasa huduma imerejea na wananchi wa eneo lake wanapata huduma ya majisafi
kwa kiwango kizuri.
Hafia Ibrahim, Mkazi
wa mtaa wa Kambangwa - Mwananyamala amesema kuwa huduma ya maji imerejea lakini
bado baadhi ya majirani hawajapata huduma na wengine wanapata kwa msukumo
mdogo.
"Tulipokea
taarifa ya kukosekana kwa huduma ya maji kutoka DAWASA kwa wiki hii mapema,
lakini kuanzia jana asubuhi (Julai 2,2025) huduma imerejea kwa msukumo mzuri.
Wananchi tunaendelea na shughuli zetu za kila siku za kijamii na kiuchumi,”
alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Bi Everlasting Lyaro amekiri kuwepo kwa
changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji kwa zaidi ya saa 10 kwa siku za
(Jumatatu hadi Jumanne), lakini kwa sasa huduma imerejea na kuwapa uhakika
wananchi wote kuwa watapata maji, huku akiwasisitiza mafundi wa Mamlaka kukesha
mtaani kufuatilia huduma.
"Mamlaka
ilitangaza matengenezo yaliyodumu kwa saa 10 na kufika siku ya Julai 2,
tuliwasha mitambo yetu ya uzalishaji maji ya Ruvu Juu na Chini na huduma kuanza
kurejea kwa wananchi. Leo tunapita mitaani kuhakikisha huduma imeimarika kwa
kiasi gani na kuangalia maeneo ambayo bado yana changamoto ili tuweze kuzitatua,” ameeleza Bi Lyaro.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano DAWASA, Bi Everlasting Lyaro
0 Maoni