Mamlaka ya Usimamizi
wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea
kuimarisha mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua
inayolenga kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta mbalimbali, hususan sekta ya
utalii.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana Julai 03, 2025 katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya
Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere (Sabasaba)
jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa TAWA, Bw. Beatus Maganja, amesema taasisi
hiyo inaendelea kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo mbalimbali ikiwemo utalii wa
picha na uwindaji wa kitalii.
“Tunawaambia
Watanzania na wawekezaji wote kwa ujumla
kuwa TAWA ni mahali sahihi kwa uwekezaji, unapotaka kuwekeza unakaribishwa
sana. Ikumbukwe kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa
na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa mazingira wezeshi Kwa wawekezaji
wote wa ndani na nje ya nchi yetu, ” alisema Maganja.
"Kama
alivyofanya Mhe. Rais na sisi tunamuunga mkono Kwa kuhakikisha kwamba fursa
hizi zinakuwa wazi Kwa wawekezaji wote na ndio maana tuko hapa kuwatangazia
waje kuwekeza katika hii taasisi," amesisitiza Afisa Habari huyo.
Aidha, Maganja
ameongeza kuwa TAWA inasimamia maeneo yenye rasilimali adimu, vivutio vya
kipekee, na mandhari ya kuvutia ambayo yanatoa fursa kubwa ya uwekezaji
endelevu kwa maslahi ya taifa na uhifadhi wa maliasili.
Bw. Maganja alitaja
baadhi ya maeneo yaliyo tayari kwa
uwekezaji kuwa ni Hifadhi ya Makuyuni Wildlife Park (Arusha), Wami-Mbiki
(Morogoro), Mpanga/Kipengere (Mbeya na Njombe), Tabora ZOO, Ruhila ZOO na
maeneo mengine mengi yenye fursa mbalimbali.
Kwa upande wake,
Afisa Mhifadhi Mkuu kutoka TAWA, Dkt. Gladson Mlay, aliwahamasisha wananchi
kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho hayo, ambapo
wanaweza kujionea wanyamapori hai wakiwemo simba, chui, fisi, mamba na spishi
mbalimbali za ndege.
Aidha, alitumia fursa
hiyo kuwaalika wananchi kuonja na kununua kitoweo cha nyamapori choma
kilichoandaliwa kwa umahiri, akisema kuwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha
matumizi ya rasilimali za maliasili kwa njia endelevu.
“Kwa wale ambao
wanasema hawajawahi Kula nyamapori choma, nyama hiyo ipo hapa, mishikaki pia
ipo na nyama ya kupeleka nyumbani nyumbani. Kwahiyo watu wote mnakaribishwa mje kuonja, Kula na kuona
kweli maliasili ni za kwetu wote” alisema Dkt. Mlay.
0 Maoni