WAZIRI MKUU, Kassim
Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza usimamizi wa
ukusanyaji wa kodi kwa wafanyabiashara ikiwemo wa mataifa ya nje walioamua kuja
kufanya shughuli zao nchini.
Amesema kuwa TRA
inapaswa kuongeza ufanisi zaidi kwenye kuwasimamia wafanyabiashara wote
kuhakikisha wanatambua sheria za ulipaji kodi pamoja na kufanya ukaguzi wa mara
kwa mara ili kuhakiki utekelezaji wake.
Ametoa agizo hilo leo
(Jumanne Julai 08, 2025) alipofungua kikao kazi cha Viongozi wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) katika kituo cha Mikutano cha Arusha (IACC).
“Nendeni mkachunguze
hawa wanaokuja kufanya biashara nchini, kama wanaondoka na mapato yetu kwa
kutolipa kodi yetu, ni lazima tubane eneo hilo kama ambavyo sisi tunabanwa
tunapokwenda kwao, yeyote aliyeamua kuja kufanya biashara Tanzania ni lazima
ajue Tanzania ina sheria zake ikiwemo za ulipaji kodi.”
Aidha, Mheshimiwa
Majaliwa ameipongeza TRA kwa kufanikiwa kukusanya Shilingi Trilioni 32.26, sawa
na ufanisi wa asilimia 103.9 dhidi ya lengo la kukusanya Shilingi Trilioni
31.05.
“Hii ni hatua ya
kihistoria na ya kujivunia kwa kuwa ni mafanikio yanayoakisi dhamira, weledi,
na juhudi mlizonazo zinazofanywa na timu ya TRA na uongozi wote katika
kuhakikisha mnafikia malengo mliojiwekea.”
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha kuendelea kufanya
maboresho ya Sera, sheria na kuimarisha mifumo ya kodi ili kufikia wigo wa juu
wa ukusanyaji kodi bila kuathiri ustawi wa shughuli za kiuchumi.
“Kwa Mamlaka ya
Mapato Tanzania, ubunifu mliouonesha mkapata mapato makubwa, endeleeni nao,
ubunifu huu umeleta mafanikio makubwa, mbinu rafiki na zakitaalamu mnazotumia
kukusanya kodi ziendelezwe, sambamba na kuzingatia Sheria, Utawala Bora, Kanuni
na utu.”
Kwa upande wake,
Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema kuwa Wizara hiyo pamoja na TRA
wamejipanga kuhakikisha Watanzania wanaelewa kuwa Maendeleo ya nchi yanatokana
na kodi.
“Wengi wanadhani kuwa
fedha za maendeleo zipo Benki Kuu, tunatakiwa kuendelea kuwaelimisha Watanzania
kwamba kila kitu cha maendeleo wanachokiona ni fedha zetu, hata fedha za mkopo
ni fedha zetu kwa kuwa tutalipa kwa kodi zetu.”
Naye Kamishna Mkuu wa
TRA Yusuph Mwenda amesema kuwa katika mwaka wa fedha ulioishia juni 30, 2025,
wameweza kuwarejeshea walipa kodi zaidi ya Shilingi trilioni 1.2 kiwango
kikubwa tangu kuanza kwa Mamlaka hiyo “Serikali imerejesha ili kuwezesha
biashara zifanye kazi.”
“Na katika mwaka huu
wa fedha tumepanga kukusanya shilingi trilioni 36 ikiwa ni mapato ghafi,
tunaamini tukiwa pamoja na walipa kodi tunafanikiwa, tunajua hii ni ndoto
ambayo viongozi wetu mnatamani tuitimize.”
0 Maoni