Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imepongezwa kwa kuendelea kusimamia kwa weledi mashauri ya madai na usuluhishi hatua ambayo imesaidia Serikali kuongeza kasi katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Pongezi hizo
zimetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Ndugu Eliakim Maswi
alipotembelea banda la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati wa Maonesho ya
Kimataifa ya 49 ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Ndugu Maswi alisema
kuwa uwepo wa weledi na ufanisi katika uendeshaji wa mashauri ya madai,
usuluhishi, Katiba, Haki za Binadamu na Uchaguzi katika Ofisi hiyo umeongeza
kasi katika kupunguza na kutatua migogoro ya kisheria kwa njia ya majadiliano
badala ya kutumia muda mrefu kusikiliza shauri hilo mahakamani.
Ameongeza kuwa fedha
zinazookolewa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zimekuwa zikitumika kujenga
miradi mikubwa ya maendeleo ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuwarahisishia
wananchi kote nchini katika kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo kwa
urahisi.
Akiitaja miradi
mikubwa inayotekelezwa nchini, ndugu Maswi amesema kuwa miradi hiyo ni pamoja
na bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha
takribani megawati 2,115 lililojengwa mto Rufiji, reli ya kisasa ya SGR, bwawa
la kidunda, vituo vya afya, miradi ya barabara, elimu, ujenzi wa meli Ziwa
Victoria pamoja na ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa unaojengwa Msalato
Jijini Dodoma.
Ameongeza kuwa
kukamilika kwa miradi hii kutachochea kasi ya wananchi katika kujiletea
maendeleo kwenye nyanja ya uchumi na kijamii kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa
kwa ujumla.
Aidha, Maswi
ameipongeza Ofisi hiyo kwa kuendelea kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa
wananchi wanaotembelea banda la Ofisi hiyo katika Maonesho ya Sabasaba kwa
lengo la kuwasaidia wananchi kuelewa haki zao na namna ya kuzitekeleza kupitia
mfumo wa kisheria ikiwemo mashauri ya madai, usuluhishi, mashauri ya katiba,
haki za binadamu na uchaguzi.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Udhibiti Ubora wa Ofisi hiyo, Bi. Mercy Kyamba
amesema kuwa ushiriki wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye Maonesho haya
ya Sabasaba ni mwendelezo wa Ofisi hii kusogeza huduma karibu na wananchi kwa
kuendelea kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi wanaotembelea banda la
Ofisi hiyo.
Bi. Kyamba ameongeza
kuwa Maonesho ya Sabasaba yatasaidia kujenga na kuongeza mahusiano na wadau
hatua itakayosaidia kutangaza majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa
taasisi za Serikali ambazo ndio wadau muhimu katika uendeshaji wa mashauri ya madai
na usuluhishi.
Maonesho ya 49 ya
kimataifa ya Kibiashara yalianza tarehe 28 Juni 2025 na kufunguliwa tarehe 7
Julai, 2025 na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dkt.
Hussein Ali Mwinyi.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Katiba na Sheria, Ndugu Eliakimu Maswi akipitia Jarida la Wakili Mkuu
alipotembelea banda la Ofisi hiyo wakati wa Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea
Jijini Dar es Salaam.
Mawakili wa Serikali
wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakiwa ndani ya banda la Maonesho la Ofisi
hiyo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wanaotembelea banda hilo wakati wa
Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Mkaguzi wa Ndani wa
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Salma Mgaya akisaini kitabu cha wageni
alipotembelea banda la Ofisi hiyo wakati wa Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea
Jijini Dar es Salaam.
0 Maoni