Waziri wa Madini, Mh.
Anthony Mavunde (Mb) amebainisha kuwa Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameelekeza kutolewa kwa leseni ya uchimbaji
madini ya nikeli kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na kwa Wachimbaji
wadogo waliokuwepo katika eneo la vilima vya Ntaka- Nachingwea,Mkoani Lindi.
Waziri Mavunde
ameyasema hayo leo tarehe 08 Julai, 2025 katika mkutano wa hadhara wa wananchi
na wachimbaji katika Kijiji cha Nditi punde tu baada ya kufanya ziara ya
kutembelea maeneo na migodi ya wachimbaji wadogo chini ya Umoja wa Vikundi vya
Wachimbaji Madini (UVIWAMA).
"Rais Dkt. Samia
S. Hassan amesikia kilio chenu cha muda mrefu cha kutaka kupewa maeneo ya
uchimbaji katika Leseni inayomilikiwa na Serikali. Na ndiyo maana nimefika hapa
kuja kuwaletea habari njema wachimbaji wadogo kwamba, hatutawaondoa katika eneo
mnalochimba na tunakwenda kuwarasimisha.”
Pamoja na kupewa eneo
la uchimbaji, naomba niwasihi wachimbaji wadogo kufuata taratibu kwa mujibu wa
Sheria ya Madini Sura ya 123 ambayo inaelekeza mwenye haki madini kuhakikisha
anapata ridhaa ya mwenye haki ardhi kabla hajaanza uchimbaji, ili kuepusha
migogoro katika shughuli zao za uchimbaji.
Rais Dkt. Samia ameelekeza
eneo la leseni hiyo lenye ukubwa wa Kilometa za Mraba 45 ipewe Shirika la
Madini la Taifa (STAMICO) kwa ajili ya kuanza uchimbaji mkubwa wa nikeli ndani
ya miezi 18 ijayo kama Sheria ya Madini inavyoelekeza.
Kwakuwa kwenye Leseni
hii serikali ililipa zaidi ya shilingi bilioni 243 kama fidia, ni lazima
sasa STAMICO na wachimbaji wadogo
wafanye uchimbaji wenye tija ili kurejesha fedha hizo katika mfuko mkuu wa
Serikali, alisema Mavunde.
Awali, akitoa salam
kwa niaba ya wachimbaji wadogo, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo Mkoa
wa Lindi (LIREMA), Bw. Mayunga Musa Buyaga amesema wachimbaji wadogo
wanamshukuru sana Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa upendo mkubwa na kuwajali na
kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kufanya uchimbaji wenye tija.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Lindi, Mh. Zainab Telack amempongeza Mh. Rais Dkt Samia kwa kurudisha matumaini
na nyuso za furaha kwa wachimbaji wadogo na kuahidi kuwa Serikali ya Mkoa
itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati ili shughuli za uchimbaji zifanyike kwa utaratibu
uliowekwa pasipo kuzalisha migogoro.
0 Maoni