Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana,
akiwa nchini Ufaransa jana Julai 8, 2025 amekutana na Mwandishi wa kitabu cha
"Tanzano-Therapie", Prof. Chantal Henry ambaye ni Mkufunzi Mwandamizi
katika Chuo Kikuu cha Paris East Creteil (UPEC) na mtaalamu wa magonjwa ya afya
akili nchini Ufaransa.
Prof. Huyo ameandika Kitabu hicho kinachozungumzia kwa
undani jinsi mtu anavyoweza kupona changamoto za saikolojia ya akili na
kuhuishwa kisaikolojia kwa kutembelea maeneo ya hifadhi na kuangalia wanyama na
vitu vya asili utafiti uliofanywa nchini Tanzania.
“Nilitembelea maeneo mengi ya kiutalii Tanzania hasa Hifadhi
za Serengeti, Ngorongoro mpaka kule Gombe-Mahale nikiwa na familia kisha
nikarudi kama mtafiti ambapo nilishiriki mimi mwenye na kuona tiba hiyo lakini
pia nimefanya mahijiano na watalii wengi.
“Nikahitimidha kwamba utalii wa kwenda maeneo hayo ya
Tanzania unatoa tiba kwa mtu mwenye hatua mbalimbali za magonjwa ya akili na
hata saikolojia ya kawaida. Tanzania ni tiba na nimekuwa nikizunguka maeneo
mengi huku Ulaya kulisema hilo na watu wameitikia kuja Tanzania,” alisema Prof.
Chantal.
Akizungumza mara baada ya mazungumzo na Profesa huyo kuhusu
kitabu hicho kilichoandikwa kwa lugha ya Kifaransa, Waziri Pindi amesema kitabu
hicho kitaendeleza kuitangaza Tanzania
na kuunga mkono kazi kubwa anayoifanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika
sekta ya utalii kupitia filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” na “Amazing
Tanzania.”
Profesa Chantal akifundisha Chuo Kikuu cha East Central
Paris na akiwa pia na kliniki ya kutibu watu wenye changamoto ya afya ya akili,
amechapisha maandiko zaidi ya 300 ikiwemo makala mashuhuri ya “Don't Forget the
Benefits of Empathy.”
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amesema
wana mshawishi Profesa huyo Kitabu hicho kitatafsiriwe pia katika lugha
mbalimbali ili watalii kutoka maeneo yote duniani waweze kukisoma na kuelewa
ikiwemo Kiingereza na Kiswahili.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini
Ufaransa Bw. Ali Mwadini ambaye ameeleza kuwa tayari kitabu hicho kwa mara ya
kwanza kilizinduliwa Ubalozini hapo Juni mwaka huu.
Waziri Chana na ujumbe wake wapo mjini Paris kuhudhuria Mkutano wa 47 wa Kamati ya Urithi wa Dunia ya Unesco ambapo taarifa mbalimbali za hali ya uhifadhi wa maeneo ya wanyamapori na malikale zikiwemo za Tanzania, zitawasilishwa.
0 Maoni