Wizara ya Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi imetoa jumla ya Hati Milki za Ardhi 1,176 wakati wa
Maonesho ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yaliyomalizika mwishoni mwa wiki.
Katika maonesho hayo
yaliyobeba kaulimbiu ya "Fahari ya Tanzania" Wizara ya Ardhi imetoa
huduma mbalimbali ikiwemo hati milki za ardhi kwa wamiliki waliokamilisha
taratibu za umiliki pamoja na utatuzi wa changamoto za sekta ya ardhi.
Akizungumza wakati wa
hitimisho la maonesho hayo jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Ardhi Msaidizi
mkoa wa Dar es Salaam anayeshughulikia wilaya ya Ilala na Temeke Rehema Mwinuka
alisema, kati ya hati hizo 1,176, hati 1,040 zimetolewa kwa wamiliki wa mkoa wa
Dar es Salaam, 68 Pwani na 68 ni kwa mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa Rehema,
wizara ya Ardhi katika maonesho hayo ya Sabasaba ilihudumia zaidi ya wananchi
1,616 waliofika kuhitaji huduma za sekta ya ardhi katika maeneo mbalimbali.
"Katika maonesho ya
mwaka huu wizara yetu ilijipanga kutoa huduma mbalimbali na imefanikiwa
kuwahudumia zaidi ya wananchi 1,616 huku hati 1,176 zikitolewa," alisema
Rehema.
Kwa upande wao, baadhi ya
wananchi waliofika Banda la Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
walionesha kuridhishwa na huduma zilizokuwa zikitolewa wakati wote wa maonesho
na kusisitiza umuhimu wa wizara ya Ardhi kuandaa huduma ya pamoja (One Stop
Center) ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma za sekta ya ardhi.
Walitolea mfano wa huduma
ya utoaji Hati Milki za Ardhi pamoja na ukadiriaji kodi ya pango la ardhi kuwa,
ni moja ya huduma iiliyopatikana kwa haraka jambo linaloonesha kuwa, wizara
ilijipanga katika maonesho hayo.
Jaji wa Mahakama Kuu
kanda ya Arusha Mhe. Aisha Bade ambaye ni mmoja wa waliopata hati milki ya
ardhi katika maonesho hayo alisema, wizara ya Ardhi kwa sasa imebadilika kwani
huko nyuma kupata hati ilichukua zaidi ya mwaka.
"Niwapongeze wizara
ya ardhi kwa hatua mliyofikia, huko nyuma kupata hati milki ya ardhi ni 'issue'
lakini leo nimeipata hati yangu ndani ya muda mfupi, hongereni sana,"
alisema.
Naye Muigizaji wa sinema
za kitanzania (Bongo Movie) Richie Mtambalike ameipongeza wizara ya ardhi kwa
kutoa huduma za papo hapo hasa utoaji wa hati milki za ardhi katika maonesho ya
kimataifa ya sabasaba.
"Niishukuru Wizara
ya Ardhi kwa kutuletea huduma hapa katika maonesho maana kwa upande wangu
nimefanikiwa kupata hati milki ya arhi hapa hapa," alisema.
Na. Munir Shemweta- WANMM
0 Maoni