Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, leo Julai 12, 2025, amefungua rasmi wa Mkutano wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri,
uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Mkutano huo
unawakutanisha Waganga Wakuu kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na
Halmashauri, ukiwa na lengo la kupitia utekelezaji wa shughuli za afya nchini,
kutathmini changamoto zilizopo, pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji
wa huduma bora za afya kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa
ufunguzi wa mkutano huo, Dkt. Mpango amesisitiza umuhimu wa uongozi thabiti
katika sekta ya afya, akiitaka timu ya viongozi hao kuhakikisha wanakuwa mstari
wa mbele katika kusimamia maadili, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali
za umma.
“Maendeleo ya taifa
lolote hayawezi kupatikana bila kuwa na wananchi wenye afya bora. Hivyo
ninawataka kuwa viongozi wa mfano katika maeneo yenu na kuweka mkazo katika
kuboresha huduma kwa wananchi, hasa maeneo ya vijijini,” amesema Dkt. Mpango.
Aidha, Makamu wa Rais
amepongeza juhudi zinazofanywa na Wizara ya Afya kupitia viongozi hao katika
mapambano dhidi ya magonjwa ya mlipuko, uboreshaji wa huduma za mama na mtoto,
pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya vituo vya afya kote nchini.
Kwa upande wake, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, amesema mkutano huo ni jukwaa
muhimu kwa viongozi wa sekta ya afya kujifunza kutoka kwa wenzao na kuja na
mbinu mpya za kukabiliana na changamoto zinazokabili utoaji wa huduma nchini.
Mkutano huo wa siku
kadhaa unatarajiwa kujadili ajenda mbalimbali zikiwemo utekelezaji wa Bima ya
Afya kwa Wote, mkakati wa Taifa wa Afya ya Msingi, usimamizi wa vifaa tiba na
dawa, pamoja na nafasi ya waganga wakuu katika kuongoza mabadiliko kwenye sekta
ya afya.
0 Maoni