Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, leo Julai 12, 2025, ameshiriki kikao
maalum cha Kundi la Afrika (Africa Group) kilichofanyika pembezoni mwa Mkutano
wa 47 wa Kamati ya Urithi wa Dunia ya Unesco unaoendelea jijini Paris,
Ufaransa.
Kikao hicho ni sehemu ya
mikakati ya pamoja ya nchi za Afrika katika kujadili na kujipanga kuhusu maeneo
ya urithi wa dunia yanayopatikana barani humo, kwa lengo la kulinda maslahi ya
Afrika wakati wa majadiliano ya pamoja na mabara mengine.
Mbali na Dkt. Abbasi,
kikao hicho pia kimehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali
J. Mwadini, pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Tanzania. Katika kikao hicho,
Dkt. Abbasi na Balozi Mwadini waliwasilisha salamu za Serikali ya Tanzania na
kutoa shukrani kwa Kamati hiyo pamoja na nchi wanachama wa Afrika kwa juhudi
wanazozifanya kusaidia nchi za bara hilo katika kulinda maeneo yao ya urithi wa
dunia.
Aidha, taarifa zinaeleza
kuwa ripoti za hali ya uhifadhi wa maeneo ya urithi wa dunia kutoka Tanzania
ambazo zilipaswa kuwasilishwa mwaka huu ikiwemo Ngorongoro, Selous na Kilwa,
tayari zimepitishwa na kuidhinishwa na vikao vya Unesco.
Mkutano wa Kamati ya
Urithi wa Dunia unaendelea jijini Paris na unatarajiwa kuhitimishwa mwishoni
mwa wiki hii, ukiwa na ajenda mbalimbali kuhusu ulinzi na uhifadhi wa maeneo ya
urithi wa dunia kutoka mataifa mbalimbali.
0 Maoni