Wawekezaji kutoka Saudi
Arabia wametembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya
49 ya Biashara ya Kimataifa ya SabaSaba, wakijionea fursa mbalimbali zilizopo
kwenye sekta ya utalii na maliasili hapa nchini.
Kiongozi wa msafara huo,
Abdulahim Ahmed, amesema wameridhishwa na juhudi za Tanzania katika kuendeleza
shughuli za utalii na uhifadhi, akibainisha kuwa kuna nafasi kubwa ya
ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia katika kukuza sekta hiyo.
“Tumefurahishwa na namna
Tanzania inavyosimamia vivutio vyake na tunatarajia kushirikiana katika
kuviboresha na kuhamasisha wawekezaji kutoka Saudi Arabia kuja kuwekeza hapa,”
alisema Ahmed.
Wakiwa katika banda la
wizara, wageni hao walipata maelezo kuhusu fursa za uwekezaji kwenye sekta za
wanyamapori, utalii na malikale, ikiwemo ujenzi wa huduma muhimu kwenye maeneo
ya vivutio.
Pia, msafara huo
ulitembelea idara mbalimbali chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, zikiwemo
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambapo walijionea shughuli za
ufugaji nyuki na bidhaa zinazozalishwa.
Aidha, wawekezaji hao
walipata maelezo kuhusu upatikanaji wa mbegu na miche bora, uwekezaji katika
mashamba ya miti, biashara ya mazao ya misitu, na matumizi ya teknolojia
kudhibiti majanga ya moto misituni.
Maonesho ya SabaSaba
yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wadau wa ndani na nje ya nchi kujadili fursa
za uwekezaji na ushirikiano, hasa kwenye sekta ya utalii na uhifadhi wa
mazingira.
0 Maoni