Wachimbaji wadogo wa
madini ya shaba wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma wametakiwa kujiunga katika
vikundi ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Mradi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), unaolenga kuwaendeleza
wachimbaji wadogo wa madini ya kimkakati, ikiwemo shaba.
Wito huo umetolewa na
Mhandisi Chacha Megewa kutoka Tume ya Madini, wakati wa utoaji wa elimu kwa
wachimbaji katika mgodi wa Minosphere, maarufu kama mgodi wa Majuto, uliopo
Kijiji cha Kitati.
Akizungumza na wachimbaji
hao, Mhandisi Megewa amesema kuwa ni muhimu wachimbaji kuunda vikundi vya
angalau watu watano, ili waweze kufikiwa kwa urahisi kupitia huduma kama
mafunzo, uunganishwaji na taasisi za kifedha, pamoja na upatikanaji wa mikopo
inayolenga kuongeza tija katika shughuli zao za uchimbaji.
“Uchimbaji salama na
wenye tija unahitaji ushirikiano na uratibu mzuri. Kupitia vikundi, wachimbaji
watapata nafasi kubwa zaidi ya kunufaika na fursa za kitaifa na kimataifa,”
amesisitiza Mhandisi Megewa.
Katika hatua nyingine,
Mhandisi huyo amepiga marufuku shughuli za ulipuaji kufanywa na mtu asiye na
cheti maalum cha ulipuaji (blasting certificate), akisema hatua hiyo ni hatari
kwa usalama wa wachimbaji na jamii inayozunguka migodi.
“Ni kosa kubwa
kuhifadhi baruti kwenye makazi ya watu. Baruti ni nyenzo muhimu, lakini
isipotunzwa ipasavyo, inaweza kuleta madhara makubwa kwa maisha, mali na
mazingira,” amesema, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia maeneo rasmi
yaliyoidhinishwa kama stoo au magazini ya kuhifadhi baruti.
Kwa upande wake,
Mkaguzi wa Migodi kutoka Tume ya Madini, Bwana Fahad Mkuu, amewataka wachimbaji
kuzingatia usalama mahali pa kazi na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea.
“Wamiliki wa migodi
wana jukumu la kuhakikisha wachimbaji wanapata vifaa kinga na mazingira yao ya
kazi ni salama. Hii itasaidia kulinda maisha yao na kuongeza ufanisi katika
shughuli za uchimbaji,” amesema.
Naye Meneja wa Mgodi
wa Minosphere, Bwana Solomon Mhina, ameishukuru Tume ya Madini kwa mafunzo
hayo, akiahidi kuyatekeleza maagizo yote yaliyotolewa kwa maslahi ya wachimbaji
na maendeleo ya mgodi.
“Tunatambua mchango
wa elimu hii kwa ustawi wa mgodi wetu na tutaendelea kushirikiana na Tume ya
Madini ili kuhakikisha usalama na tija kwa wachimbaji
wetu,” amesema Mhina.


0 Maoni