Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Dar es Salaam wamefanya ukaguzi wa ujenzi na matengenezo ya barabara katika mkoa huo unaolenga kuhakikisha miradi inakamilika kwa viwango na kwa wakati.
Meneja wa TARURA mkoa
wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga amesema kuwa, wametembelea wilaya ya
Temeke ambapo walikagua barabara mbalimbali ikiwemo barabara ya kwa Diwani na
zile zinazotekelezwa chini ya mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es Salaam awamu
ya pili (DMDP).
“Tumeona maendeleo
mazuri kwenye utekelezaji, Mkandarasi yupo kazini na tunatarajia kujenga zaidi
ya Km 7.2 katika eneo la makazi na biashara, ambapo magari makubwa na malori
hupita mara kwa mara. Barabara zinajengwa kwa kiwango cha zege ili kukidhi mahitaji
ya shughuli za kiuchumi zinazofanyika," amesema Mkinga.
Pia alitembelea
barabara ya Yombo yenye urefu wa Km 1.6, ambapo ujenzi unaendelea kwa kiwango
cha zege katika maeneo ya wazi pamoja na kipande cha mita 600 kinachojengwa kwa
kushirikiana na Manispaa ya Temeke.
“Ninamshukuru Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kwa
kuwezesha upatikanaji wa fedha za matengenezo. Hii imerahisisha utekelezaji wa
barabara ya Yombo na ile ya Dkt. Omar. Kipande cha mita 600 kinachojengwa chote
kwa zege.” ameongeza.
Meneja Mkinga pia
alitembelea barabara ya Tuangoma–Masaki yenye urefu wa Km 3.9, eneo ambalo
awali lilikuwa na changamoto kubwa ya mvua na udongo laini uliokuwa
ukisababisha kukatika kwa mawasiliano.
“Hili ni eneo la
mchanga, mvua ikinyesha tu hakuna mawasiliano kabisa. Mkandarasi anayetekeleza
mradi huu anafanya kazi chini ya mkataba wenye thamani ya Shilingi bilioni 27.
Mradi unahusisha pia ujenzi wa vivuko vya Chaulembo ambavyo vimepangwa kwa
mujibu wa maelekezo ya viongozi wa mkoa,” amesema.
Akiwa eneo la Chamaruba,
ameeleza namna mvua kubwa za Aprili na Mei zilivyoharibu miundombinu na kufunga
kabisa mawasiliano kati ya pande mbili za mtaa huo. Hata hivyo, kwa ushirikiano
na viongozi wa Serikali ya Mtaa na Serikali Kuu, fedha za dharura zilitolewa
ili kujenga makalavati matano na kurudisha mawasiliano.
Kwa upande wao,
wananchi wa maeneo hayo walitoa shukrani zao kwa Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi hiyo ambayo
imeleta unafuu mkubwa kwa wananchi.
“Awali ilikuwa
tunapata shida kuwavusha watoto kwenda shule, hadi mzazi umpeleke mtoto na umrudishe. Wakati mwingine wagonjwa
walihitaji kubebwa hadi upande wa pili. Lakini sasa hivi, tuna daraja, tuna
barabara, tuna amani, tunaishukuru serikali," amesema mmoja wa wakazi wa
eneo la Chamaruba.



0 Maoni