Samia ampa Dkt. Kimambo maagizo mazito kuiongoza Muhimbili

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Delilah Kimambo kuhakikisha anaendeleza ubora wa huduma na kuimarisha uongozi wa hospitali hiyo kongwe na ya kimkakati katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumza leo Juni 28, 2025 katika viwanja vya Ikulu Chamwino mkoani Dodoma wakati wa kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, Rais Samia amesema Muhimbili inahitaji uongozi wa kitaalamu na wa kiutawala ili kuendelea kutoa huduma bora za kibingwa na kuimarisha utalii wa tiba.

“Muhimbili inahitaji professionalism na administrative skills. Nimepitia wasifu wa watu wengi lakini nikaona wewe Dkt. Delilah Kimambo ndiyo unafaa kuiongoza hospitali hiyo. Nenda kaendeleze pale alipoishia Prof. Janabi,” amesema Rais Samia.

Katika hotuba hiyo, Rais Samia amemwelekeza Dkt. Kimambo kuhakikisha huduma zinazotolewa na Muhimbili zinaendelea kukidhi viwango vya kimataifa, sambamba na kusimamia kikamilifu matumizi ya rasilimali zilizowekezwa na Serikali kwa ajili ya kuboresha hospitali hiyo.

Amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuimarisha vifaa tiba vya kisasa na kuleta wataalamu wa juu, ili kuiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma bora kwa Watanzania na wageni wanaokuja kupata matibabu nchini.

Aidha, Rais Samia amesema tayari Serikali imepata fedha kwa ajili ya maboresho ya zaidi katika hospitali hiyo, hususan kwenye ujenzi wa miundombinu ya majengo mapya, ikiwa ni muendelezo wa juhudi za kuboresha sekta ya afya nchini.

Dkt. Delilah Kimambo aliteuliwa na Rais Samia tarehe 16 Juni, 2025 kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, kuchukua nafasi ya Prof. Mohamed Janabi ambaye amehamishiwa katika majukumu mengine ya kitaifa.

Hospitali ya Taifa Muhimbili ni miongoni mwa taasisi muhimu za tiba nchini na inatajwa kuwa kiongozi wa huduma za kibingwa na utalii tiba katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.



Chapisha Maoni

0 Maoni