Wananchi wilayani Karagwe mkoani Kagera wameeleza kunufaika na ujenzi wa barabara ya Nyakahanga-Nyabiyonza -Masheli ambapo kero ya usafiri iliyokuwepo imeondolewa baada ya matengenezo ya maeneo korofi.
Akiongea katika
mahojiano maalum, Diwani wa Kata ya
Nyakahanga, Mhe.Charles Beichumila ameeleza kuwa kipindi cha masika wananchi wa
kata za Nyakahanga na Nyabiyonza walikuwa hawawezi kuwasiliana kutokana na hali
mbaya ya barabara.
"Tunamshukuru
Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na mbunge wetu Mhe. Innocent Bashungwa kwa
utatuzi wa kero hii ya muda mrefu maana kwa sasa barabara inapitika kwa kipindi
chote cha mwaka," amesema Mhe. Beichumila.
Kwa upande wake,
Meneja wa TARURA wilaya ya Karagwe, Mhandisi Kalimbula Malimi amesema kuwa
kipaumbele katika matengenezo ya barabara hiyo yenye urefu wa Km 96 kilikuwa ni
kuanza na maeneo korofi kwa kuweka tabaka la lami na kwamba hatua itakayofuata
ni kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami.
"Tumeanza na
maeneo korofi kwa kuweka tabaka la lami ambapo hadi sasa tayari Km 9.2
zimekamilika na wananchi wanapita bila usumbufu," amesema Mhandisi
Kalimbula.
Kwa upande wake, Bw.
Josam Pastory mkazi wa kata ya Nyakahanga ameeleza kuwa kero kubwa iliyokuwepo
ni hasa kipindi cha masika ambapo akina mama walishindwa kufika hospitalini
huku watoto wakishindwa kufika shuleni kwa urahisi.
Wakala ya Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Karagwe inaendelea na utekelezaji wa
miradi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya usafiri na
usafirishaji kwa urahisi.
0 Maoni