Wavuvi wa Jimbo la Musoma Vijijini Mkoani Mara wameanza kupata matunda mazuri kutokana na uvuvi wa samaki kwa kutumia vizimba, ambao Mbunge wa Jimbo hilo, Prof. Sospeter Muhongo amekuwa mstari wa mbele kuhimiza uvuvi huo katika Ziwa Victoria.
Wakiongea kwa nyakati
tofauti mmoja wa wavuvi walionufaika na uvuvi wa samaki kwa kutumia vizimba
katika Kijijini Kigera, Kitongoji cha Kurukiri amesema anavuna samaki takribani
Tani 40 kutoka kwenye vizimba vyake 4 vyenye upenyo wa mita 10.
Amesema masoko ya
samaki wanaovunwa kutoka kwenye vizimba yapo, ambayo ni ya walaji na viwanda
vya minofu ya samaki. “Bei inaendana na ukubwa na uzito wa samaki, na kwa sasa
ni kati ya Shilingi 7,000 na 10,000 kwa kilo moja.”
Samaki waliovuliwa jana
katika Kizimba cha Ziwani Kurukiri, Kijijini Kigera, Kata ya Nyakatende waliuzwa
kwa kiasi cha shilingi 8,500 kwa kilo.
Jimbo la Musoma
Vijijini lenye jumla ya Kata 21, lina Kata 18 zilizoko pembezoni mwa Ziwa
Victoria. Kwa hiyo, uvuvi ni kazi inayoajiri watu wengi wa Jimboni mwetu.
Wataalamu wa uvuvi wa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wakiwemo wa TAFIRI, walishirikiana na NEMC kubaini
maeneo mazuri yanayokidhi vigezo vya kufanya uvuvi wa vizimba ndani ya Jimbo
letu.
Mbali ya mikopo nafuu
iliyotelewa na Serikali yetu kwenye uvuvi wa vizimba, Mbunge wa Jimbo la Musoma
Vijijini, Prof Sospeter Muhongo anaendelea kuwashawishi wavuvi wa jimboni kwake
kwenda Benki za CRDB na NMB kuchukua
mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya uvuvi wa vizimba. Mbunge huyo
ameishawasiliana na Benki hizo mbili kuhusu mikopo hiyo.
Wavuvi na wananchi wa
Jimbo la Musoma Vijijini wanaendelea kutoa shukrani nyingi kwa Mhe Rais Dkt
Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha njia, kwa vitendo, ya uwekezaji mkubwa kwenye
uvuvi wa vizimba nchini mwetu.
0 Maoni