Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) umeanza rasmi kutumia ndege nyuki (drones) kwa ajili ya
kuimarisha ulinzi wa misitu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kisasa wa
kukabiliana na vitendo haramu vinavyoathiri rasilimali za misitu nchini.
Hatua hiyo imezinduliwa
jana, Juni 2, 2025, katika viwanja vya Ofisi ya Kanda ya Kusini ya TFS mkoani
Mtwara, ambako ndege hizo zilifanyiwa majaribio mbele ya maafisa wa uhifadhi na
marubani waliopata mafunzo ya kuziongoza.
Akizungumza kwa niaba
ya Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu Tanzania, Prof. Dos Santos Silayo, Kamanda wa
Kanda ya Kusini, Manyisye Mpokigwa, alisema matumizi ya drones ni hatua muhimu
ya kimkakati katika kuimarisha ufuatiliaji wa maeneo ya misitu na kuongeza
ufanisi wa kazi za doria na ulinzi.
“Teknolojia hii
itaongeza uwezo wetu wa kubaini kwa haraka uhalifu wa kimazingira unaoendelea
ndani ya misitu, ikiwemo uvunaji haramu wa mbao, uchomaji moto wa misitu,
utengenezaji haramu wa mkaa, pamoja na uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa
matumizi ya kilimo au makazi,” alisema Mpokigwa.
Aliongeza kuwa
matumizi ya ndege hizo yataongeza tija katika shughuli za uhifadhi kwa
kurahisisha doria katika maeneo magumu kufikika, kukusanya taarifa kwa usahihi
kupitia kamera za kisasa zenye uwezo wa kuona hata usiku au kwenye maeneo yenye
uoto mnene, na kupunguza gharama za ulinzi ikilinganishwa na mbinu za kawaida.
“Mbali na kupunguza
gharama za mafuta na nguvu kazi, teknolojia hii pia itasaidia kuwalinda
wahifadhi kwa kuepusha hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa doria za ana kwa
ana,” alieleza.
Mpokigwa aliwataka
wahifadhi wa ngazi ya wilaya kote nchini kutumia fursa hiyo kwa weledi, ili
kuhakikisha usalama na uendelevu wa misitu ya Tanzania unalindwa kwa kutumia
maarifa ya kisasa.
“Huu ni wakati wa
kutumia teknolojia kama silaha mpya ya kulinda misitu yetu. Wahifadhi wanapaswa
kuwa mbele katika matumizi ya drones ili kutambua waharibifu mapema na kuchukua
hatua kabla athari hazijatokea,” alisisitiza.
0 Maoni