Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa
Majaji kutoka nchini Ghana na Nigeria ulioko nchini kwa lengo la kujifunza na kubadilishana
uzoefu wa masuala mbalimbali yanayohusu
Sheria.
Mwanasheria Mkuu wa
Serikali amekutana na ujumbe huo tarehe 2 Juni, 2025 katika Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.
Akizungumza mara
baada ya kukutana na Ujumbe huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa
Ujumbe huo umekuja nchini kufanya ziara ya mafunzo kuhusiana na masuala ya kisheria hususani
kazi mbalimbali zinazotekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Tumepokea ugeni
kutoka nchini Ghana ambao unaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Ghana
ameambatana na timu yake pamoja na majaji kutoka Nigeria ambao wamekuja
kujifunza juu ya masuala mbalimbali yanayotekelezwa na Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali,” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa ujumbe huo umeambatana na Taasisi ya GIZ
inayosimamia mradi wa kuchapisha sheria, maamuzi pamoja na kanuni mtandaoni
ujulikanao kama TanzLII, ambapo aliishukuru taasisi hiyo kwa kutekeleza mradi
huo na amewaahidi kuendelea kuuhudumia mfumo mara baada ya mradi huo wa TanzLII
kukamilika.
“Tunawashukuru sana
GIZ kwa kuhakikisha kwamba sheria zetu tunaziweka kwenye mfumo wa TanzLII hivyo
kurahisisha katika utoaji wa huduma mbalimbali za kisheria, na sisi tunawaahidi
kuendelea kuutumia mfumo,” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake, Jaji
Jennifer Dadzie kutoka Mahakama ya Rufani nchini Ghana, ameishukuru Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mapokezi mazuri waliyoyapata na ziara hiyo
imekuwa na mafanikio makubwa kwakua wameweza kujifunza namna Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali inavyotekeleza majukumu yake.
“Lengo la ziara hii
ni kujifunza na kubadilishana uzoefu juu ya masuala ya kisheria yanavyoendeshwa hapa Tanzania,
tumetembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na tumeweza kujifunza na
kuona Ofisi hii inavyotekeleza majukumu yake,” amesema Jaji Dadzie.
0 Maoni