Katibu Mkuu wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema kitabu
alichoandika Alhaj Mzee Mohamed Mustafa Songambele kitakuwa mojawapo ya rejea
adhimu za historia ya Tanzania.
Balozi Nchimbi
amesema kuwa kitabu hicho kiitwacho “Safari ya Karne”, kina utajiri wa maelezo
kuhusu mapambano ya kutafuta uhuru wa Tanganyika, kupatikana kwa nchi na taifa
la Tanzania na kuundwa kwa CCM.
Dkt. Nchimbi amesema
hayo alipokuwa akitoa salaam za pole na rambirambi kwenye msiba wa Hayati Alhaji Mzee
Songambele, akimwakilisha Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mjini Songea, mkoani Ruvuma, leo Jumatatu
tarehe 2 Juni 2025.
“Kutokana na heshima
na mchango mkubwa wa Mzee Songambele kwa nchi yetu, taifa letu na chama chetu,
Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuguswa sana na msiba huu, ameniagiza
rasmi kumwakilisha na ameagiza Chama na Serikali kuchukua gharama zote za msiba
huu.
“Mzee Songambele
amefariki akiwa amemaliza kuandika kitabu chake. Hadi mwezi Machi mwaka huu,
alikuwa amekiita jina la “Swahiba wa Nyerere”, lakini miezi miwili iliyopita
akabadili, nadhani aliona atatimiza miaka 100, akakiita “Safari ya Karne,”
amesema Balozi Nchimbi na kuongeza;
“Kutokana na umuhimu
wa kitabu hicho, ambacho aliniomba niandike dibaji na niliandika, humo
ameelezea mengi kuhusu yeye na Nyerere, harakati za uhuru, utaifa wetu na CCM
pia, Chama Cha Mapinduzi kitasimamia ili kitabu hicho kitoke ili Watanzania
wapate kujifunza historia vizuri,” alisema Balozi Nchimbi.
Aidha, Balozi Nchimbi
alisema Mzee Songambele pia alikuwa mmoja wa viongozi waliotoa mchango mkubwa
kwa nchi, taifa, chama na serikali kutokea Mkoa wa Ruvuma, akisisitiza kuwa
hilo ni jambo linalostahili kuenziwa na viongozi wa kizazi cha sasa kwa kuwa
waadilifu, wanaowajibika, wazalendo kwa nchi na kuwatumikia watu.
Hayati Alhaji Mzee
Songambele, mwanasiasa na kiongozi mkongwe nchini, ambaye alifariki usiku wa
kuamkia Jumapili ya tarehe 1 Juni, mwaka huu, alizikwa Jumatatu Juni 2, 2025
katika makaburi ya familia yaliyoko Bombambili, mjini Songea.
0 Maoni