Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua Mkakati wa Taifa wa
Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia, pamoja na Kampeni ya Kitaifa ya
Uhamasishaji na Uelimishaji kuhusu Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia lengo
likiwa ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya
kupikia na hivyo kuwezesha asilimia 80 ya Watanzania kuhamia katika matumizi ya
Nishati Safi ya Kupikia ifikapo 2034.
Akizindua Mkakati huo
wa Mawasiliano jijini Dodoma, Juni 2, 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza kuwa mkakati huo usiishie kukaa kwenye
makabati bali utekelezwe katika ngazi zote za Serikali hadi ngazi ya mtaa bila
kusahau Sekta binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na vyombo vya Habari kuwa
mstari wa mbele katika kuutekeleza.
Katika uzinduzi huo,
Dkt. Biteko amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara namba
moja wa matumizi ya Nishati safi ya kupikia ndani na nje ya nchi ambapo kutoka
azindue Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia (2024-2034)
mnamo tarehe 08 Mei, 2024 matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini
yameongezeka kutoka asilimia 6 hadi 16.
“ Katika kuthibitisha
jinsi anavyolipa umuhimu suala hili la Nishati Safi ya Kupikia, Mheshimiwa Rais
pia ameunda Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia ambacho kina jukumu maalumu la
kusimamia ajenda ya nishati safi ya kupikia na kwa kupitia kitengo hiki
Serikali itaendelea na shughuli mbalimbali ikiwemo kubuni na kusimamia miradi,
pia kusimamia kampeni zote za Kitaifa za uelimishaji na uhamasishaji wa nishati
safi ya kupikia,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ameeleza
kuwa, matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia yanaendelea kuathiri afya na
maisha ya watumiaji wengi hasa kina mama na watoto chini ya umri wa miaka
mitano ambapo taarifa zinaonesha kuwa, watu bilioni 2.1 sawa na asilimia 24.7
ya Watu wote Duniani hawana nishati safi ya kupikia ambapo kati yao watu Milioni 990 sawa asilimia 47.1
ya wanaotumia nishati isiyo salama wanatoka barani Afrika.
Ameeleza kuwa, Afrika
inalazimika kufunga mkanda katika safari ndefu ya kuelekea kwenye matumizi ya
Nishati Safi ya Kupikia ambapo kwa upande wa Tanzania amesema kuwa kila Taasisi
inapaswa kutambua na kutekeleza jukumu lake kikamilifu.
Dkt. Biteko
amewasisitiza Wadau wote wanaohusika na Nishati Safi ya Kupikia kuhakikisha
kuwa wanandaa na kutekeleza Kampeni zinazolenga makundi maalum katika jamii,
kukuza uelewa wa umma kuhusu njia za ufadhili na gharama nafuu, kuhakikisha
ujumbe thabiti wenye kueleweka unafika kwa wadau wote na kuendeleza na
kuimarisha njia za mawasiliano za kuaminika.
Katika hatua
nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia Kitengo cha Tathmini
na Ufuatiliaji kufanya tathmini katika kila robo mwaka ili kuweza kujipima juu
ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amempongeza Rais, Dkt. Samia kwa
kuendelea kuonesha kuwa nishati safi ya
kupikia si suala la maneno bali ni vitendo na ndio maana anatambulika duniani
kama kinara wa nishati safi ya kupikia.
Amesema kuwa suala la
Nishati Safi ya Kupikia ni kipaumbele cha Mkoa wa Dodoma ambapo juhudi
mbalimbali zinachukuliwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia
akitoa mfano kuwa kwa Mkoa wa Dodoma kwa sasa tayari magereza 9 yanatumia
nishati safi ya kupikia, shule za VETA 3 na shule 9 za bweni huku kazi ya
uhamasishaji ikiendelea.
Naibu Waziri wa
Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema katika kipindi cha miaka minne sekta ya
Nishati imekuwa mashuhuri kwa masuala mbalimbali kubwa likiwa ni nishati safi
ya kupikia na kueleza kuwa nguvu ya ushawishi ya Rais, Dkt.Samia imefanya
ajenda ya nishati safi ya kupikia kukubalika ndani na nje ya nchi na hivyo
kutoa hakikisho la usalama wa afya za wananchi na mazingira pia.
Ameongeza kuwa
Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia uliozinduliwa utaongeza kasi
za programu za nishati safi ya kupikia na kuleta mapinduzi ya kuhama kutoka
matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia kwenda kwenye nishati safi ya
kupikia.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuzinduliwa kwa Mkakati wa Taifa
wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia ni hatua muhimu katika utekelezaji wa
Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Ameeleza kuwa Mkakati
huo umeandaliwa na Wizara ya Wizara ya
Nishati kwa kushirikiana na Shirika la
Maendeleo la Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) chini ya ufadhili wa Umoja wa
Ulaya (EU) ambapo Mkakati huo unaongozwa na kaulimbiu ya kitaifa isemayo
“Nishati Safi ya Kupikia, Okoa Maisha na Mazingira.”
Amesema lengo kuu la
mkakati ni kuongeza uelewa wa wananchi na taasisi kuhusu umuhimu wa matumizi ya
nishati safi ya kupikia na malengo mengine mahususi ni kuandaa na kutekeleza
kampeni maalum za uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia,
kuhakikisha ujumbe wenye lengo la pamoja unafika kwa wadau wote pamoja na
kuendeleza na kuimarisha njia za mawasiliano.
Naye, Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. David Mathayo amempongeza
Rais, Dkt. Samia kwa kuanzisha gurudumu la Nishati Safi ya Kupikia, pia
amempongeza Dkt. Biteko kwa jinsi anavyoongoza Wizara na kutoa ushirikiano kwa
kamati hiyo.
Aidha, Mwakilishi wa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa
Serikali, Rodney Thadeus amesema kuwa Wizara hiyo itahakikisha mkakati wa
mawasiliano uliozinduliwa unatekelezwa kwa mafanikio kwa kushirikiana na Wizara
ya Nishati pamoja na wadau wengine vikiwemo vyombo vya Habari.
Vilevile, Mshauri wa
Rais ( Nishati Safi ya Kupikia na Maendeleo ya Jamii) Angellah Kairuki
amepongeza juhudi za serikali katika kuimarisha matumizi ya nishati safi ya
kupikia huku kielelezo mojawapo kikiwa ni uzinduzi wa mkakati wa mawasiliano
ambao ni muhimu katika kufikisha ujumbe kwa umma kuhusu umuhimu wa matumizi ya
nishati safi ya kupikia.
Naye, Lamine Diallo,
Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali kutoka Umoja wa Ulaya ( EU), ameipongeza Wizara
ya Nishati kwa tukio hilo muhimu la kuzindua Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati
Safi ya Kupikia na kusema kuwa inaonesha kwa vitendo juhudi za Serikali katika
kuboresha maisha ya wananchi kupitia Nishati Safi ya Kupikia.
0 Maoni