Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kuwakaribisha wananchi katika banda lake
maalum kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yanayoendelea katika
Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma, ambapo pamoja na
mambo mengine, unatoa huduma ya tiba ya kudungwa na nyuki (api-therapy) bure
kabisa kwa wananchi.
Huduma hiyo ni sehemu
ya juhudi za TFS kuwaelimisha Watanzania juu ya manufaa ya uhifadhi wa
mazingira kupitia njia za asili. Kwa mujibu wa Mhifadhi Brenda Mwakipesile
kutoka Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Vikindu, huduma hiyo inalenga kuimarisha
kinga ya mwili, kupunguza maumivu ya viungo, kuboresha mzunguko wa damu, na
kusaidia afya ya akili.
“Tumeileta huduma hii
bure kwa wananchi ili kuwaonesha kuwa uhifadhi wa misitu hauishii kwenye miti
pekee, bali pia unaweza kuzaa tiba za asili ambazo ni salama na zenye manufaa
ya kiafya,” alisema Mhifadhi Brenda.
Kwa upande wake, Mkuu
wa Banda la TFS katika maonesho hayo, Mhifadhi Mkuu Kassim Ally, alisema
ushiriki wa taasisi hiyo katika maadhimisho ya mwaka huu unaendana na kaulimbiu
ya kitaifa isemayo “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa – Dhibiti
Matumizi ya Plastiki.”
“TFS tunashiriki kama
wadau wakuu wa uhifadhi, tukionesha namna misitu inavyoweza kutumika kwa njia
endelevu, kuanzia elimu ya mazingira, huduma za afya, matumizi ya malisho kwa
mifugo, hadi uzalishaji wa miche ya miti,” alisema Ally.
TFS inawahimiza
wananchi wote kujitokeza kushiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Mazingira
Duniani yanayoendelea hadi Juni 5, 2025, kwa lengo la kujifunza, kufurahia, na
kupata huduma za kipekee zitolewazo na wataalamu wa uhifadhi wa misitu.
Naibu Katibu Mkuu
(Muungano), Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi, akipatiwa
huduma ya tiba ya kudungwa na nyuki (api-therapy) kutoka kwa Mhifadhi Brenda
Mwakipesile wa TFS – Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Vikindu, katika viwanja vya
JKCC, Dodoma. Huduma hiyo inalenga kuimarisha kinga ya mwili kwa kutumia tiba
asilia kutoka kwenye mazingira ya misitu, ikiwa ni sehemu ya kuonesha mchango
wa uhifadhi katika afya na utalii wa Mazingirq. Huduma hiyo inatolewa bure kwa
wananchi wote wanaotembelea banda la TFS.
0 Maoni